IQNA

Sala ya Ijumaa marufuku tena Morocco baada ya kuenea corona

19:32 - September 21, 2020
Habari ID: 3473191
TEHRAN (IQNA) – Wizara ya Wakfu ya Morocco imetangaza kupiga marufuku tena swala za Ijumaa nchini humo kutokana na kuenea tena kwa kasi ugonjwa wa corona au COVID-19 nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa, Ahmad Tawfique, Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu Morocco ametangaza kuwa: “Hali ya corona nchini humo hairuhusu tena Swala za Ijumaa kuendelea kuswalia katika misikiti kwani msongamano wa watu utapelekea kuongezeka maambukizi ya ugonjwa huo.”

Amesema iwapo swala za Ijumaa zitaruhusiwa tena, hilo litawezekana tu kwa sharti la kuzingatia sheria kali za afya ikiwa ni pamoja na kupima kiwango cha joto cha waumini wote kabla hawajaingia msikitini na waumini kutokaribiana wakati wa swala. 

Halikadhalika Waziri wa Wakfu Morocco amesema kuswalia tena swala za Ijumaa misikitini kutategemea kumalizika ugonjwa wa corona au kupungua idadi ya maambukizi kiasi cha kutokuwepo hatari kwa waumini wanaofika msikitini. Wanaharakati wa Kiislamu wamekuwa wakiishinikiza serikali ya Morocco iruhusu swala za jamaa na ijumaa nchini humo ziendelee kama kawaida lakini serikali imekataa kusalimu amri.

Hadi sasa watu 102,000 wameambukizwa corona nchini Morocco na miongoni mwao 1,830 wamefarikia dunia.

3923994

captcha