IQNA

Ibada ya Umrah kuanza tena katika awamu nne

17:47 - September 23, 2020
Habari ID: 3473197
TEHRAN (IQNA) – Saudi Arabia imesema itawaruhusu Waislamu walioko nchini humo kutekeleza Ibada ya Umrah kuanzia Oktoba Nne.

Katika taarifa Jumanne, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia imesema Ibada ya Umrah itaanza tena baada ya kufungwa kwa zaidi ya miezi minne sasa kutokana na janga la COVID-19.

Taarifa hiyo imesema idhini imetolewa ya kuwaruhusu waumini kutekeleza Umrah ambapo wataruhusiwa tu kufika katika Msikiti Mtakatifu wa Makka kuanzia Oktoba 4, 2020 kwa kuzingatia kanuni zote za afya. Umrah itaanza kwa awamu nne, ya kwanza itaanza Oktoba nne ambapo raia wa Saudia na raia wa kigeni wanaoishi nchini humo wataruhusiwa kuzuru Msikiti Mtakatifu wa Makka kwa kiwango cha asilimi 30 ya uwezo wa msikiti huo, kwa siku.

Baadaye kuanzia Oktoba  18 idadi hiyo itafika asilimia 75 na kisha asilimia 100 kuanzia Novemba mosi.

Bado hakuna taarifa zozote kuhusu kuwaruhusu wageni kutoka nje ya nchi kuanza kuingia Saudia kwa ajili ya Umrah.

Hadi kufikia Septemba 23, watu 331,000 walikuwa waeambukizwa COVID-19 nchini Saudia na 4,542 wameshafariki kutokana na ugonjwa huo hadi sasa. Wizara ya Afya ya Saudia imesema hivi sasa kiwango cha maambukizi kimepungua kwa asilia 88 mwezi huu ikilinganishwa na mwezi Juni.

3472614

captcha