IQNA

Matumaini baada ya kutiwa saini mapatano ya kusitisha vita Libya

21:21 - October 24, 2020
Habari ID: 3473292
TEHRAN (IQNA) - Hatimaye baada ya mazungumzo marefu na tata pande hasimu nchini Libya zimetiliana saini makubaliano ya usitishaji vita.

Pande hizo kuu hasimu ambazo ni Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya na wanamgambo wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar, jana Ijumaa zilitiliana saini huko Geneva Uswisi makubaliano ya usitishaji vita chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Stephanie Williams Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Libya amesisitiza kuwa, kamati mbili za pamoja za kijeshi zinaoundwa na ujumbe unaofungamana na Serikali ya Mwafaka ya Tripoli na ule wenye mfungamano na Khalifa Haftar zimefikia makubaliano ya kusitisha vita. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, wanajeshi wote wa nchi ajinabi wanapaswa kuondoka Libya katika kipindi cha miezi mitatu na kwamba makubaliano hayo yatarejesha usalama na amani nchini humo. 

Usimamizi wa Umoja wa Mataifa

Makubaliano ya kudumu ya kusitisha vita nchini Libya yamefikiwa na pande hasimu kwa usimamizi wa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika hali ambayo, zaidi ya mwezi mmoja uliopita, kulifikiwa makubaliano ya muda ya usitishaji vita baina ya pande hizo. Katika kipindi hicho, wawakilishi kutoka mashariki na magharibi mwa Libya waliendelea na mazungumzo yao huko Morocco na Uswisi yaliyokuwa na lengo la kuhitimisha mgogoro wa ndani wa nchi hiyo na kuchora ramani ya njia kwa ajili ya muundo wa kisiasa kwa mustakabali wa nchi. Duru zote hizo za mazungumzo ambazo zilisimamiwa na Umoja wa Mataifa hatimaye matunda yake yameonekana baada ya pande hasimu za kisiasa nchini Libya kutiliana saini Ijumaa ya jana makubaliano ya kudumu ya usitishaji vita na mapigano.

Kidhahiri ni nukta nzuri

Kufikiwa makubaliano ya kudumu ya usitishaji vita nchini Libya, kidhahiri inaonekana kuwa nukta nzuri ya kuanzia katika mchakato wa kisiasa na kijeshi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, ambayo ilitumbukia katika lindi la vita na mapigano ya ndani tangu mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.

Hata hivyo mapigano yaliyoanza mwezi Aprili mwaka uliopita baina ya wangambao wa Khalifa Haftar wanaojiita jeshi la taifa na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa yalikuwa ya umwagaji damu mkubwa zaidi. Vita hivyo si tu kwamba vilichukua mkondo mpana zaidi, bali kwa kuzingatia uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya Libya, viligeuka na kuwa uwanja wa mapambano baina ya madola hayo ambapo kila mmoja aliiuunga mkono upande fulani akitanguliza mbele maslahi yake. Hali hiyo ilifanya vita hivyo kuzidi kuchukua mkondo mpana na tata zaidi siku baada siku na kulikuwa na kibarua kigumu cha kufikia makubaliano ya usitishaji vita hasa kutokana na kuwa, hilo lilikuwa likingana na maslahi ya madola husika huko Libya.

Fauka ya hayo, kuenea virusi vya Corona nchini Libya na matokeo hasi ya virusi hivyo, kuendelea mapigano kulikabiliwa changamoto nyingi na ulazima wa kupelekewa misaada ya kibinadamu wananchi walioathiriwa na vita nalo likayafanya matatizo ya Libya kuwa maradufu.

Madola ya kigeni

Kwa kuzingatia kuwa kivitendo wanamgambo wanaoongozwa na Khalifa Haftar pamoja na kupata misaada mingi kutoka kwa mataifa kama Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Saudi Arabia, Russia na Ufaransa wameshindwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kufikia malengo yao makuu yaani kuiondoa madarakani Serikali ya Mwafaka wa Kiataifa yenye makao yake katika mji mkuu Tripoli na ambayo inatambuliwa na jamii ya kimataifa, ingawa hilo nalo lina sababu zake kama vile himaya ya kila upande ya kilojistiki na kijeshi ya Uturuki na himaya ya kifedha ya Qatar, pande mbili za vita hivyo zimefikia natija hii kwamba, mgogoro wa sasa wa Libya hauwezi kupatiwa ufumbuzi kwa mtutu wa buunduki. Pande hizo zimefikia natija hii kwamba, ufumbuzi wa kisiasa kupitia Umoja wa Mataifa ndio njia pekee ya kuinasua Libya kutoka katika kinamasi ilichokwama ndani yake. 

Azma imara

Ni kwa msingi huo ndio maana, Mkuu wa Timu ya Mazungumzo ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa anasema kuwa, makubaliano hayo yatakuwa chimbuko la amani na uthabiti wa ardhi ya Libya. Ni kwa muktadha huo pia ndio maana pande mbili hasimu nchini Libya zimetaka makubaliano hayo yawasilishwe katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kupasishwe azimio la kulazimisha usitishaji wa kudumu wa machafuko kwa pande zote. Inaonekna kuwa, kinyume na huko nyuma ambapo ama makubaliano yaliyofikiwa hayakutekelezwa au haukupita muda yalikiukwa, mara hii pande hizo hasimu zinaonekana kuwa na azma na irada thabiti ya usitishaji wa kudumu wa vita na kuendeleza mazungumzo ya kisiasa baina yao. Hadi kufikia sasa pande mbili zimekutana katika duru mbili za maziungumzo nchini Morocco na zimesisitiza kuendeleza mazungumzo hayo ili kuhakikisha kuwa, kunafikiwa makubaliano ya mwisho baina yao.

3472919

captcha