IQNA

Wapalestina wamlaani Rais wa Ufaransa kutokana na sera zake dhidi ya Uislamu

19:40 - October 25, 2020
Habari ID: 3473295
TEHRAN (IQNA) - Makundi ya kupigania ukombozi Palestina yamemlaani Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kutokana na hatua yake ya kuunga mkono michoro ya kikatuni yenye kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Sami Abu Zuhri, amesema msimamo wa Macron wa kuunga mkono vitendo vya kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW ni  katika fremu ya njama ya kuhuisha tena vita vya msalaba.

Nayo harakati ya Jihad Islamu imesema kuuvunjia heshima Uislamu na Mtume Muhammad SAW ni mstari mwekundu na Waislamu hawawezi kustahamili tena hali hii.

Mapema mwezi huu na katika mwendelezo wa sera za kupiga vita Uislamu nchini Ufaransa, Emmanuel Macron alizindua mpango wa eti kulinda thamani za kisekulari za nchi hiyo dhidi ya kile kilichotajwa kama "Misimamo Mikali ya Kiislamu".

Rais wa Ufaransa alidai kuwa Uislamu ni dini iliyo "kwenye mgogoro" ulimwengu mzima, matamshi ambayo yamewaghadhabisha Waislamu kote duniani.

Emmanuel Macron pia ameunga mkono kitendo kiovu cha jarida la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na kusisitiza kuwa, Ufaransa itaendelea kuchapisha vibonzo hivyo. Macron amedai kuwa huo ni uhuru wa kujieleza.

3472925

captcha