IQNA

Indhari ya UN kuhusu hali mbaya sana ya watoto wa Yemen

11:02 - October 28, 2020
Habari ID: 3473302
TEHRAN (IQNA) - Sehemu za Yemen zinakabiliwa na kiwango kikubwa cha utapiamlo kwa watoto, na nchi hiyo inaelekea kwenye baa kubwa la mgogoro wa usalama wa chakula.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo ambayo imesema utapiamlo umeongezeka zaidi miongoni mwa watoto mwaka huu kutokana na janga la COVID-19. Ripoti hiyo imebaini kuwa, kushuka kwa uchumi, mafuriko, kuongezeka migogoro na kupungua kwa ufadhili wa shughuli za msaada ni kati ya sababu zingine ambazo zimezidisha hali ya njaa nchini humo baada ya takriban miaka sita ya vita vya Saudia dhidi ya Yemen.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Yemen, Lise Grande amesema tangu mwezi Julai wameonya kwamba Yemen inakaribia kutumbukia kwenye janga kubwa la mgogoro wa usalama wa chakula. Ameongeza kwamba ikiwa vita havitomalizwa hivi sasa katika taifa hilo basi itaelekea kwenye hali ambayo haitoweza kubadilishwa na kuingia kwenye hatari ya kupoteza kizazi kizima cha watoto nchini humo.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Machi 2015 Saudi Arabia, ikiungwa mkono na  Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu  na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande nchi hiyo. Moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake nchini Yemen hadi sasa umeshasababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Uvamizi wa kijeshi wa Saudia umeisababishia pia nchi masikini ya Yemen uhaba mkubwa wa chakula na dawa.

3472957

captcha