IQNA

Rais wa Iran atuma salamu za pongezi kwa mnasaba wa Maulidi ya Mtume SAW

16:30 - November 03, 2020
Habari ID: 3473324
TEHRAN (IQNA)- Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia ujumbe marais wa nchi za Kiislamu akiwapongeza kwa mnasaba wa kuadhimisha Maulidi na siku ya kuzaliwa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu na Nabii wa rehma, upendo na amani, Muhammad SAW.

Jumbe hizo zimetumwa kwa mnasaba wa siku ya leo tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal inayosadifiana na siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad (saw).

Katika jumbe tofauti aliowatumia marais na viongozi wa nchi za Kiislamu, Rais Hassan Rouhani amesema kuwa, sira na mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) daima ni tochi inayowamulikia wanadamu katika vipindi vyote vya giza na kuwaelekeza kwenye vilele vya juu kabisa vya masuala ya kiroho na kibinadamu. Rais Rouhani amesisitiza kuwa: Kufuata njia na mienendo ya Mtume SAW na kupata auni ya Qur'ani na muujiza wake wa mbinguni vinaweza kuwa ufunguo wa wanadamu katika kuwajihiana na aina mbalimbali za matatizo, hitilafu na mizozo ya dunia ya leo.

Katika ujumbe huo uliotumwa kwa marais na viongozi wa nchi za Kiislamu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kuwa: Mtume Muhammad SAW ni ruwaza njema ya maadili na rehma kwa walimwengu wote; na hapana shaka kuwa kumtusi na kumvunjia heshima mtu adhimu kama huyu ni kuvunjia heshima matukufu, maadili na uhuru; na vilevile kuwatetea na kuwakingia kifua watu wanaomtusi na kumvunjia heshima ni kuunga mkono na kutetea uovu, uchafu na uchupaji mipaka. 

Rais Rouhani amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu inalaani vikali vitendo kama hivyo na kuongeza kuwa: Inatarajiwa kuwa nchi za Kiislamu pia zitalaani hatua kama hizo zinazopingana na akili na mantiki. 

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake wa Maulidi ya Mtume kwa viongozi wa nchi za Kiislamu, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema anatarajia kwamba dunia itaweza kuvuka salama kipindi kigumu cha sasa cha maambukizi ya virusi vya corona kwa kusaidiana; na wanadamu wote, husuan mataifa ya Kiislamu, wapate tena afya na maisha bora.

/3932939

captcha