IQNA

Hatimaye Msikiti wa kwanza katika mji mkuu wa Ugiriki wafunguliwa

19:17 - November 04, 2020
Habari ID: 3473329
TEHRAN (IQNA)- Msikiti wa kwanza katika mji mkuu wa Ugiriki, Athens umefunguliwa baada ya miaka 14 ya vuta nikuvute na urasimu kupita kiasi.

Swala ya kwanza katika msikiti huo imeswaliwa Jumatatu wakati wa Ishaa kwa uzingatiwaji kanuni za kiafya za kuzuia maambukizi ya corona. Ni waumini wachache tu waliohudhuria tukio hilo.

Kwa kufunguliwa msikiti huo, sasa mji wa Athens hautakuwa na sifa ya mji mkuu pekee wa Umoja wa Ulaya usio na msikiti.

Imamu wa kwanza wa msikiti huo ni Zaki Mohammad, raia wa Ugiriki mwenye asili ya Morocco.

Msikiti huo, ambao moja ya masharti ya ujenzi wake ni kuwa, usiwe na mnara, una uwezo wa kupokea waumini 500.

Waislamu Ugiriki kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka ujengwe msikiti mjini Athens ili kuweza kukidhi mahitaji ya jamii ya Waislamu wanaozidi kuongezeka.

Katika hali ya hivi sasa Waislamu wapatao laki tano wanakadiriwa kuishi nchini Ugiriki ambapo wengi wana asili ya Uturuki. Katika miaka ya hivi karibuni Waislamu kutoka Afrika, Asia ya Kati, Mashariki ya Kati na kusini mwa Asia wamekuwa wakihamia nchini humo kwa sababu tofauti. Wengi wa Waislamu laki mbili wanaoishi katika mji mkuu Athens pia wanatoka katika nchi za Afghanistan, Bangladesh, Misri, Nigeria na Pakistan.
Mgogoro wa kujengwa msikiti mkuu mjini Athens unarudi nyuma hadi katika miaka ya 1930. Mji wa Athens haujakuwa na msikiti mkuu na rasmi tokea utekwe na jeshi la Othmania mwaka 1833.

3473023

captcha