IQNA

Matumaini ya Guterres kuhusu kuboreka hali ya Waislamu Warohingya baada ya uchaguzi Myanmar

17:08 - November 07, 2020
Habari ID: 3473338
TEHRAN (IQNA) – Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea matumaini yake kuwa uchaguzi mkuu wa Novemba 8 nchini Myanmar utaandaa mazingira ya kurejea nyumbani mamia ya maelefu ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Antonio Guterres amesema ana matumaini kuwa Warohingya wakimbizi watarejea Myanmar na kupata usalama na heshima. Katika taarifa Ijumaa, ameelezea matumaini yake kuwa uchaguzi huo utaeleta maendeleo endelevu na jumuishi, haki za binadamu na mabadiliko ya kidemokrasia.

Itakumbukwa kuwa wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa. Aidha zaidi ya Waislamu wengine milioni moja wa jamii hiyo walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh huku wengine wakipata hifadhi katika nchi kama vile India, Thailand na Malaysia.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein aliesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Mwezi Januari mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) iliitaka serikali ya Myanmar kuchukua hatua za dharura za kuzuia mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Rohingya, ikisisitiza kuwa Warohingya hao wamesababishiwa machungu na maumivu yasiyoweza kufutika au kurekebishika.

3473046

captcha