IQNA

UN:Yemen inaelekea katika maafa makubwa zaidi duniani

21:38 - November 21, 2020
Habari ID: 3473379
TEHRAN (IQNA) – Yemen, ambayo inakabiliwa na hujuma ya kijeshi ya Saudia, sasa inaelekea katika baa kubwa zaidi la njaa kuwahi kushuhudiwa duniani kwa miongo kadhaa, ametahadharisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Katika taarifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha upinzani wake kwa  uamuzi wowote wa Marekani ambao unalenga kuiwekea vikwazo Harakati ya Ansarullah, ambayo wapiganaji wake hulisaidia Jeshi la Yemen katika kukabiliana na hujuma ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo.

Guterres amesema Ijumaa kuwa, wafanyakazi wa kutoa misaada wamebainisha wasi wasi wao kuwa, iwapo Marekani itaitangaza Harakati ya Ansarullah kuwa ni ‘kundi la kigaidi’, hatua hiyo itaathiri vibaya jitihada za kufikisha misaada ya dharura Yemen.

Guterres amesema iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa, mamilioni ya watu watapoteza maisha Yemen.

Nchi hiyo maskini ya Kiarabu inasumbuliwa na maafa makubwa zaidi ya kibinadamu duniani baada ya miaka kadhaa ya vita na mapigano.

Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen. 

3473171

Kishikizo: yemen saudia
captcha