IQNA

Maandamano London kupinga jinai za UAE nchini Yemen

22:06 - December 03, 2020
Habari ID: 3473418
TEHRAN (IQNA) – Maandamano yamefanyika nje ya ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mjini London, Uingereza kulaani jinai za UAE nchini Yemen.

Katika maandamano hayo yaliyofanyika kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya UAE, waandamanaji wamesema UAE haina chochote cha kusherehekea katika siku hiyo kwani ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu nchini humo. Aidha waandamanaji wamesema UAE imetekeleza jinai za kivita Yemen, Libya na kwingineko.

Waandamanaji wametaka Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi Mohamed Bin Zayed afikishwa kizimbani ajibu mashtaka ya jinai za kivita Yemen na ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

Jumatano  Wakuu wa Yemen walitoa tahadhari kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayozidi kuwa mbaya nchini humo kutokana na vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu ambapo 'mtoto mmoja wa Yemen hupoteza maisha kila dakika 10'.

Aidha Jumanne pia Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimepelekea zaidi ya watu 233,000 kupoteza maisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Machi 2015 Saudi Arabia, ikiungwa mkono na  Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu  na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro wa kila upande nchi hiyo.

Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen.

3473303

Kishikizo: uae yemen saudia
captcha