IQNA

Wabunge wa Iran walaani uamuzi wa Marekani wa kuwekea vikwazo Chuo Kikuu cha al-Mustafa SAW

21:55 - December 28, 2020
Habari ID: 3473501
TEHRAN (IQNA)- Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) imelaani vikali hatua ya serikali ya Marekani ya kukiwekea vikwazo Chuo Kikuu cha Kimataifa cha al-Mustafa cha Iran.

Katika taarifa ya jana Jumapili, Wabunge 175 wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu wamesema kuiwekea vikwazo taasisi hiyo ya elimu ya juu ya Iran kwa mara nyingine tena kumedhihirisha sura halisi ya sera za kiistikbari za dola la kibeberu la Marekani.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, kitendo hicho kimeonesha ni jinsi gani utawala wa Washington unavyoionea gere taifa la Iran kwa kupiga hatua katika nyuga za sayansi na utamaduni.

Wabunge hao wa Iran wameitaja hatua hiyo ya Marekani ya kukiwekea vikwazo Chuo Kikuu cha Kimataifa cha al-Mustafa cha Iran ambacho kaulimbiu yake ni 'haki, umaanawi na mantiki' kama kitendo kiovu, ghalati, kisichofaa na haramu.

Itakumbukwa kuwa, Disemba 9 mwaka huu, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza kukiwekea vikwazo chuo hicho cha Kimataifa cha Jamiatul Mustafa, ukiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa sera zake za kupinga ustawi wa elimu, sayansi na utamaduni duniani.

Chuo hicho kilitoa taarifa ya kulaani hatua hiyo ya Marekani na kubainisha kuwa, kitendo cha kuiwekea vikwazo taasisi ya kielimu ambayo ni mwanachama rasmi wa Jumuiya ya Vyuo Vikuu vya Kimataifa Duniani na ambayo wanachuo wake wanatambulika duniani kama wahamasishaji wa uadilifu na kuzuia vitendo vya uchupaji mipaka hakina maana nyingine isipokuwa ni kupinga elimu.

3943649

captcha