IQNA

Maulamaa wa Kiislamu duniani walaani hatua za Ufaransa dhidi ya Uislamu na Waislamu

15:31 - January 25, 2021
Habari ID: 3473587
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu (IUMS) imelaani vikali hatua ambazo serikali ya Ufaransa inachukua dhidi ya Waislamu.

Katibu Mkuu wa IUMS Sheikh Ali Mohiuddin Ali Al-Qaradaghi ametoa taarifa na kuitaka serikali ya Ufaransa iache mara moja kuingilia mambo yanayohusiana na Uislamu na iamileiane na Uislamu kama inavyoamilliana na dini nyinginezo nchini humo.

Amesema uamuzi wa hivi karibuni wa Ufaransa kufunga misikiti kadhaa au kuweka vizingiti katika shughuli za misikiti ni ukiukwaji wa uhuru wa kidini.

Sheikh Al-Qaradaghi ametoa wito kwa wasomi wa dini zinginezo Ufaransa kupinga ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Wiki iliyopita, kamati maalumu ya Bunge la Kitaifa la Ufaransa liliidhinisha sheria ya 'thamani za jamhuri' ambazo zilipendekezwa na rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na kile alichokitaja ni 'Uislamu wa wanaotaka kujitenga.'

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin amedai katika ukurasa wake wa Twitter kuwa sheria hiyo inalenga kulinda thamani za jamhuri sasa na siku za usoni.

Jumuiya ya Waislamu Ufaransa (CFCM) imepinga vikali sheria hiyo na kuitaja kuwa yenye kuwawekea Waislamu vizingiti katika maisha yao yote.

Sheria hiyo inaipa serikali haki ya kuingilia mambo ya misikiti na kupeleleleza kamati zinazosimamia misikiti na pia kudhibiti matumizi ya pesa za misikiti na asasi za Waislamu.

 3949634

captcha