IQNA

Saudia: Chanjo ya COVID-19 itakuwa lazima kwa kila anayeenda Hija

15:42 - March 02, 2021
Habari ID: 3473695
TEHRAN (IQNA)- Wakuu wa afya nchini Saudi Arabia wametangaza kuwa kila Mwislamu ambaye anapanga kutekeleza Ibada ya Hija ni sharti athibitishwe kuwa amepata chanjo dhidi ya COVID-19 au corona.

Katika taarifa Jumanne, Wizara ya Afya ya Saudia imesema chanjo hiyo ya corona itakuwa sharti la kushiriki katika ibada ya Hija baada ya waziri wa afya nchini humo. Tangazo hilo limekuja baada ya Waziri wa Afya wa Saudia  Tawfiq Al Rabiah kunukuliwa na gazeti la Al-Madinah akisema kuwa kupata chanjo ya corona ni sharti la kushiriki katika ibada ya Hija.

Amesema hatua za mapema zimeshaanza kuchukuliwa kwa ajili ya kuimarisha vituo vya afya katika miji mitakatifu ya Makka na Madina pamoja na maeneo yote ambayo yanatumiwa kama njia ya kuingia Mahujaji ili kufanikisha ibada ya Hija.

Hatahivyo taarifa hiyo ya Wizara ya Afya ya Saudia haikuweka wazi iwapo ibada ya Hija mwaka huu itajumuisha mahujaji kutoka nje ya ufalme huo. Mwaka jana, kutokana na maambukizi ya corona, kulikuwa na Mahujaji chini ya 10,000 ambao wote walikuwa ni wakaazi wa Saudia wakiwemo raia wa kigeni.  

Hadi sasa watu 377,000 wameambukizwa corona nchini Saudia na miongoni mwao 6,500 wamepoteza maisha.

Ufalme huo ulianza kampeni ya chanjo ya corona mnamo Disemba 17 na ingali inaendelea.

3480356

captcha