IQNA

Kiongozi Muadhamu atuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Sheikh al-Zein wa Lebanon

7:51 - March 04, 2021
Habari ID: 3473701
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemtumia ujumbe wa rambirambi Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kufuatia kuaga dunia Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Maulamaa Waislamu Lebanon.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu siku ya Jumatano alimtumia ujumbe Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon  na kumpa ujumbe wa rambi rambi kufuatia kuaga dunia mwanazuoni wa kijihadi Kadhi Sheikh Ahmed al-Zein ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Maulamaa Waislamu Lebanon. Katika ujumbe huo, Kiongozi Muadhamu ametuma salamu za rambi rambi kwa maualmaa,  familia, maashiqi na wanafunzi wa mwanazuoni huyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wake amesema mwendazake alitetea Harakati ya Imam Khomeini MA kwa uwajibikaji na kitaalamu. Aidha amesema Sheikh al-Zein kwa muda mrefu alipambana dhidi ya mrengo wa uistikbari na Uzayuni na alikuwa katika safu ya mapambano ya mataifa ya eneo dhidi ya Uistikbari. Halikadhalika amesema mwanazuoni huyo wa Lebanon hatasahaulika katika historia ya muqawama na mapambano katika eneo.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: "Kwa mara nyingine natuma salamu zangu za rambi rambi kwa watu wa Lebanon na hasa waliokuwa pamoja naye na pia wanamapambano wenzake katika Jumuiya ya Mualamaa Waislamu Lebanon. Namuomba Mwenyezi Mungu amrehemu na amghufurie."

Senior Lebanese Cleric Passes Away  

Sheikh al-Zein, aliyeaga dunia Jumanne, alikuwa miongoni mwa wanazuoni maarufu wa Ahlu Sunna nchini Lebanon na pia aliwahi kuwa jaji au kadhi katika mahakama ya mji wa Sidon.

Aidha alikuwa maarufu kwa misimamo yake imara dhidi ya utawala wa Kizayuni na alisisitiza kuwa mapambano ni njia pekee ya kuuangamiza utawala huo.

/3957509

captcha