IQNA

Watu 20 wauawa katika hujuma ya kigaidi Mogadishu, Somalia

19:44 - March 06, 2021
Habari ID: 3473710
TEHRAN (IQNA)- Watu wasiopungua 20 wameuawa na wengine 30 wamejeruhiwa katika shambulio la kigaidi la mripuko wa bomu lililotegwa garini uliotokea nje ya mkahawa mmoja ulioko karibu na bandari katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Kwa mujibu wa mashuhuda na chombo rasmi cha habari cha serikali moshi mkubwa ulitanda angani na milio ya risasi ilisikika baada ya shambulio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo.

Dokta Abdulkadir Aden, mwasisi wa shirika la utoaji huduma za magari ya kubebea wagonjwa la AAMIN amevieleza vyombo vya habari kuwa wameondoa maiti 20 na majeruhi 30 katika eneo la tukio.

Shambulio hilo la kigaidi lililofanywa na mtu aliyejitolea mhanga limetokea nje ya mkahawa wa Luul Yemeni ulioko karibu na bandari.

Mkazi wa eneo hilo Ahmed Abdullahi amesema: "Gari iliyokuwa ikiendeshwa kwa mwendo wa kasi iliripuka kwenye mkahawa wa Luul Yemeni. Nilikuwa naelekea mkahawani hapo lakini nilirudi mbio baada ya mripuko kutoa mtikisiko na moshi kutanda katika eneo."

Japokuwa hadi sasa hakuna aliyetangaza kuhusika na shambulio hilo, lakini msemaji wa polisi ya Somalia Sadiq Ali Adan amelihusisha shambulio hilo na kundi la kigaidi la Ash-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, ambalo hufanya mashambulio ya aina hiyo dhidi ya mji mkuu Mogadishu.

Kwa akali, jengo moja lililoko karibu na mkahawa wa Luul Yemeni, ambao ulishambuliwa pia mwaka uliopita, limeporomoka baada ya mripuko huo wa jana usiku na inahofiwa kuna watu wamekwama kwenye kifusi cha jengo hilo.

Mripuko huo wa shambulio la kigaidi ulitokea wakati wa chakula cha usiku ambapo mkahawa huo ulikuwa umejaa watu.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 baada ya kuangushwa utawala wa Siad Barre. Katika miaka ya hivi hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wa al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wanaokadiriwa kufikia 21,000 wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa al-Shabab. Hatahivyo pamoja na vitihada hizo za kimataifa, magaidi wa al-Shabab wanaendelea kutekeelza hujuma Somalia na nchi jirani ya Kenya.

3474173

Kishikizo: somalia ugaidi
captcha