Kwa mujibu wa tovuti ya albayan, Kituo cha Kimataifa Fatuwa cha Al Azhar, kimechapisha taarifa katika ukurasa wake wa Facebook na kusema kwa kuzingatia kuwa chanjo ya Corona haiingizwe mwilini kupitia mdomo au pua basi haibatilishi Saumu.
Aidha kituo hicho kimesema chanjo ya Corona haitambuliwa kuwa ni aina ya chakula au kinywaji na inatumika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa hivyo haibatilishi Saumu.
Pamoja na hayo, Kituo cha Fatwa cha Al Azhar kimependekeza kuwa, iwapo Mwislamu atadungwa chanjo ya Corona katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani basi adungwe baada ya Futari. Hii ni kwa sababu yamkini mwenye kudungwa chanjo ya Corona akahitajia lishe ya haraka kutokana na athari za chanjo hiyo.
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unatazamiwa kuanza Aprili 12 2021 kwa kutegemea mwezi mwandamo.