IQNA

Rais wa Tunisia afika Libya baada ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa

18:08 - March 17, 2021
Habari ID: 3473743
TEHRAN (IQNA) –Rais Kais Saied wa Tunisia leo ametembelea nchini ya Libya ambapo amefnaya mazungumzo na viongozi wa serikali mpya ya umoja wa kitaifa.

Rais wa Tunisia afika Libya baada ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifaAkiwa nchini Libya, Rais wa Tunisia amekutana na waziri mkuu wa muda  wa serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya, Hamid Dbeibah, ambaye ana jukumu la kuandaa uchaguzi kabla ya mwezi Disemba.

Safari ya Saied inalenga kuonyesha uungaji mkono wa Tunisia kwa mchakato mpya wa kidemokrasia nchini Libya.

Hatimaye baada ya miezi kadhaa ya mivutano na kuainisha hatima ya siasa za Libya, Mawaziri wa Serikali ya Muda ya Umoja wa Kitaifa waliapishwa Jumatatu katika Bunge la nchi hiyo huko katika mji wa Tobruk.

Aguilla Saleh Issa, Spika wa Bunge la Libya amesema kuwa, kufanyika hafla ya kuapishwa mawaziri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni hatua muhimu kwa ajili ya kurejesha demokrasia katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Spika wa Bunge la Libya ameitaka serikali hiyo kuanza kazi zake mara moja.

Kuanza kazi Serikali ya Muda ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, ni kufunguliwa ukurasa mpya wa maisha ya kisiasa nchini humo. Libya imekuwa ikishuhudia vita, machafuko na mivutano ya kisiasa tangu mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi. Anga hiyo iliandaa uwanja wa uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kila moja kati ya madola hayo kutaka hisa katika uga wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo hususan maliasili na vyanzo vya utajiri vya Libya. Kushadidi hitilafu za ndani huko Libya na uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni kumeigeuza Libya na kuwa medani ya vita vya niaba vya madola ya kigeni kiasi kwamba, weledi wengi wa mambo walitoa indhari kuhusiana na kugawanyika nchi hiyo.

3474274

Kishikizo: libya tunisia
captcha