IQNA

Katika mazishi ya aliyekuwa rais wa Tanzania, Magufuli

Rais Kenyatta wa Kenya awavutia wengi baada ya kusitisha hotuba wakati wa adhana

22:34 - March 22, 2021
Habari ID: 3473754
TEHRAN (IQNA) - Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amewavutia wengi baada ya kusimaisha hotuba yake kwa zaidi ya dakika moja kupisha wito wa swala (adhana) ya adhuhuri wakati akihutubu leo katika shughuli ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli mjini Dodoma.

Wakati akianza kutoa salamu zake katika Uwanja wa Uhuru katika mji mkuu wa Tanzania,  Dodoma adhana ilisikika kutoka katika msikiti uliopo karibu na uwanja huo na punde baada ya kusikia sauti ya adhana, Kenyatta alisitisha kwa muda kutoa hotuba yake na adhana ilipomalizika aliendelea na maelfu ya waombolezaji waliokuwa uwanjani hapo walimpigia makofi.

Kitendo hicho cha Rais Kenyatta kimewavutia wengi katika mitandao ya kijamii, hasa Waislamu, ambao wamempongeza kwa kuheshimu matukufu ya Kiislamu.

Katika hotuba yake Kenyatta amemuomba Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuendeleza falsafa ya 'Hapa Kazi Tu' aliyoiacha Magufuli kwa kuwa inawafanya Watanzania kuwa na moyo wa ushujaa na kusonga mbele. Amesema Dkt. Magufuli amelifunza bara la Afrika kuwa linaweza kustawi na kuimarika bila kutegemea misaada ya nchi ajinabi.

Viongozi na marais kutoka nchi 17 duniani hususan za Afrika wamehudhuria shughuli hiyo ya kitaifa ya kumuaga mwendazake Magufuli.

Magufuli alifariki dunia Machi 17 kutokana na maradhi ya moyo. Rais huyo wa awamu ya tano anatarajiwa kuzikwa Machi 26 nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

Nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa makamu wake, Bi Samia Suluhu Hassan ambaye amepata umashuhuri kwa kuwa rais wa kwanza mwanamke Afrika Mashariki na pia amewavutia wengi duniani kwa kuwa anazingatia vazi la staha la Kiislamu, Hijabu.

3964444

 

captcha