IQNA

Kiongozi wa Ansarullah: Ni wajibu na jukumu la kidini la Umma wote wa Kiislamu kupambana na Wazayuni

12:53 - May 07, 2021
Habari ID: 3473884
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kukabiliana na vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel ni wajibu na jukumu la kidini la Umma wote wa Kiislamu.

Abdul-Malik al-Houthi amesema hayo katika hotuba aliyoitoa jana Alkhamisi kwa njia ya televisheni, kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds inayoadhimishwa leo katika ulimwengu wa Kiislamu, bali hata katika mataifa yanayopenda haki na uadilifu duniani.

Amesema, "Sisi, kama ulimwengu wa Kiislamu, tuna wajibu mbele ya Allah wa kuchukua hatua za kuwaunga mkono Wapalestina na kuzima tishio la adui."

Ameeleza bayana kuwa, adui Mzayuni si adui kama adui mwingine, lakini ndiye adui mwenye uhasama zaidi kwa Umma wa Kiislamu. Amefafanua kuwa, utawala huo pandikizi ulizaliwa kutokana na jinai na mauaji ya kimbari, na umetenda uhaini mkubwa wa mauaji ya kuogofya dhidi ya Wapalestina na Umma wote wa Kiislamu.

Kiongozi huyo wa harakati ya Houthi ya Yemen amebainisha kuwa, Wazayuni wanaitakidi kuwa Waislamu hawastahiki haki yoyote ya kibinadamu.

Abdul-Malik al-Houthi amekosoa baadhi ya mataifa ya Kiislamu na Kiarabu kwa kutolipa uzito unaostahili suala la Palestina. Amesema madola hayo yamekataa kuzipa msaada na kuziunga mkono harakati za muqawama katika eneo kama Hamas katika Ukanda wa Gaza na Hizbullah ya Lebanon.

3474641

captcha