IQNA

Waislamu Kenya walalamika baada ya Saudia kuzuia Hija

14:02 - June 22, 2021
Habari ID: 3474030
TEHRAN (IQNA) – Waislamu wa Kenya wamebainisha malalamiko yao baada ya kubainika kuwa hawataweza kutekeleza Ibada ya Hija mwaka huu baada ya Saudi Arabia kutangaza kupiga marufuku Mahujaji kutoka nje ya ufalme huo.

Hassan Ole Naado mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya (Supkem), amethibitisha kuwa amepokea taarifa rasmi kutoka Saudia kuwa Wakenya na Waislamu wa maeneo mwengine duniani hawataruhusiwa kuingia Saudia kutekeleza Ibada ya Hija mwaka huu wa 2021.

Ole Naada amewataka Waislamu Kenya kumuomba Mwenyezi Mungu awawezeshe kutekeleza Ibada ya Hija mwakani.

Waislamu wengi Kenya wanasema Saudia haina haki ya kuchukua maamuzi ya upande mmoja kubatilisha Ibada ya Hija bali ingepaswa kushauriana na viongozi wa Kiislamu kote duniani.

 Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, ibada ya Hija mwaka huu itafanyika kwa kushirikisha raia na wageni wanaoishi nchini humo wasiozidi elfu 60.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudia imesema mahujaji hao elfu 60 kutoka ndani ya nchi wanalazimika kwanza kupata chanjo ya virusi vya corona kabla ya kushiriki katika ibada ya Hija ya mwaka huu.

Wizara hiyo pia imeshurutisha watu wanaotaka kushiriki ibada ya Hija mwaka huu wasiwe na matatizo sugu ya kiafya na wawe na umri wa kati ya miaka 18 hadi 65.

Wizara ya Hija ya Saudia imetetea uamuzi huo kwa kusema kuwa, sheria za dini ya Uislamu zinalipa umuhimu mkubwa suala la kulinda nafsi za wanadamu.

3475010/

Kishikizo: hija waislamu kenya
captcha