IQNA

Kiongozi Muadhamu : Kuwategemea Wamagharibi hakuna faida yoyote

20:04 - July 28, 2021
Habari ID: 3474136
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mipango na miradi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipaswi kufungamanishwa na ushirikiano na nchi za Magharibi, kwani imedhihirika wazi wakati wa kipindi cha serikali inayomaliza muda wake hapa nchini kwamba, kuwategemea Wamagharibi hakuna faida yoyote.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumatano katika mkutano wake na Rais Hassan Rouhani anayemaliza muda wake uongozini na baraza lake la mawaziri katika Husseiniya ya Imam Khomeini (MA) katikati mwa Tehran.

Kiongozi Muadhamu ameeleza bayana kuwa, "uzoefu kutoka serikali ya sasa umeonesha kuwa, Wamagharibi si tu hawana muamana, lakini wanatafuta fursa yoyote itakayojitokeza kulidhuru taifa la Iran."

Amesema kuwaamini Wamagharibi hakujazaa matunda yoyote katika serikali ya awamu ya 11 na 12 iliyoongozwa na Dakta Rouhani na kusisitiza kuwa, hili linapaswa kuwa funzo muhimu la kuzingatiwa.

Ayatullah Ali Khamenei amemhutubu Rais Rouhani na maafisa wa serikali yake kwa kusema: Kila wakati mlipoweka pembeni masuala ya kitaifa kwa ajili ya kufanya mazungumzo na nchi za Magharibi na Marekani, hamukuweza kusonga mbele, bali mlikwama. Ameongeza kuwa, "wakati wote ambapo mliamua kusimama kidete na kutowategemea wala kuwaamini Wamagharibi, mlipata mafanikio."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kuwa, Iran ni nchi ya kimapinduzi, na tangu baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran limesimama kidete mkabala wa mazito na hatari, sambamba na kujaribu kulinda thamani na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei ameashiria ahadi hewa za Magharibi juu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kubainisha kuwa, "Wamarekani walidai kuwa wataondoa vikwazo, lakini badala yake wameiwekea Iran masharti katika mazungumzo ya nyuklia. Hii inamaanisha kuwa, wanaandaa mazingira ya kuhujumu zaidi JCPOA pamoja na miradi ya makombora (ya Iran) na masuala ya eneo."

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa pongezi, kheri na fanaka kwa Waislamu wote kote duniani, kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya Idd ya Ghadir.

3986977

captcha