IQNA

Nukta kadhaa kuhusu kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky nchini Nigeria

19:34 - July 30, 2021
Habari ID: 3474142
TEHRAN (IQNA)- Mahakama Kuu ya Jimbo la Kaduna nchini Nigeria Jumatano ilifutilia mbali tuhuma zote alizobambikiziwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na mkewe, na kutoa amri ya kuachiliwa kwao mara moja.

Mahakama hiyo imesema tuhuma zote zilizowasilishwa na mwendesha mashtaka wa serikali dhidi ya Sheikh hazikuwa na mashiko yoyote wala kuthibitishwa kisheria. Sheikh Zakzaky na mke wake wamekuwa kizuizini kwa zaidi ya miaka minne kutokana na tuhuma zisizo na msingi, kwa mujibu wa mawakili wake.

Hukumu ya Mahakamu Kuu ya Kaduna ni ushindi sio kwa Sheikh Zakzaky na mkewe Zinat Ibrahim tu bali kwa jamii nzima ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Wawili hao wamekuwa kizuizini tangu kutekelezwa na jeshi la Nigeria jinai ya Zaria mwaka 2015 hadi sasa. Tarehe 13 Disemba 2015, jeshi hilo lilitekeleza jinai hiyo ya kutisha katika Husseiniyya ya Swahib az-Zaman ambapo wafuasi wa Ahlul Bait wa Mtume walikuwa wamekusanyika kuomboleza na kukumbuka kifo cha Imam Hussein (AS) ambaye ni mjukuu mpendwa wa Mtume Mtukufu (SAW), ambapo liliua na kujeruhi watu wasiopungua 2000. Sheikh Zakzaky alijeruhiwa vibaya katika ukandamizaji huo wa jeshi la Nigeria ambao ulimpelekea kupoteza jicho lake moja na kudhoofisha pakubwa la pili.

Mateso gerezani

Mbali na ukandamizi huo, Sheikh Zakzaky na mkewe waliandelea kupata mateso mengi wakiwa kizuizini ambapo walinyimwa hata huduma ya msingi kabisa ya matibabu. Katika kipindi hiki chote serikali ya Nigeria ilitumia kila mbinu kumlazimisha Sheikh akubali tuhuma alizobambikiziwa lakini licha ya mateso hayo yote, mwanamapambano huyo aliendelea kusimamam imara na kushikilia misimamo yake ya kidini.

Wafuasi chini ya mashinikizo

Katika kipindi cha Sheikh Zakzaky kuwa kizuizini, Mashia na wafuasi wake walikabiliwa na mashinikizo makubwa kutoka kwa serikali ya Abuja ambapo sherehe na marasimu yao yote ya kidini kama maomblezo ya Ta'sua na Ashura yalipigwa marufuku. Ni wazi kuwa serikali ya Nigeria imekuwa akitoa mashinikizo na kuwatesa Mashia kwa ajili ya kupunguza na hata ikiwezekana kufutilia mbali kabisa shughuli zao za kiutamaduni, kisiasa, kijamii na kidini.

Uchochezi wa ajinabi

Tunaweza kusema kuwa mashinikizo na mateso hayo yalitokana na uchochezi wa baadhi ya nchi ajinabi au za kigeni ambazo zinachukulia shughuli zozote za kidini na Kiislamu kuwa ni sawa na ugaidi unaoendeshwa na makundi ya kigaidi kama Boko Haram. Hii ni katika hali ambayo shughuli zinazoendeshwa na Sheikh Zakzaky na kundi lake la Harakati ya Kiislamu ya Nigeria zinatofautiana kabisa na za makundi ya kitakfiri na kigaidi kama Boko Haram, ambayo yana uhusiano na mfungamano wa moja kwa moja na magaidi wa Daesh.

Saudia na Israel

Ni wazi kuwa Nigeria ambayo ina watu wengi zaidi barani Afrika na iliyo na utajiri mkubwa wa maliasili yakiwemo mafuta na gesi ni moja ya nchi muhimu za bara hilo inayokodolewa macho ya tamaa na nchi za kigeni. Suala hilo limewapelekea washirika wawili wakuu wa Marekani Asia Magharibi yaani Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel kuizingatia zaidi nchi hiyo ya Kiafrika na kufanya juhudi kubwa za kupenya na kuwashawishi viongozi wake wakubaliane na kutekeleza siasa zao za kieneo na hasa za kuwakandamiza Mashia.

Omar Zaki, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nigeria anasema: Serikali ya Nigeria imepewa na Saudia jukumu la kupambana na Mashia wa nchi hii na kufutilia mbali ushawishi wa Sheikh Zakzaki miongoni mwa watu wa nchi hii. Wana wasi wasi na hata kusambazwa habari zinazohusiana na shaksia huyu mashuhuri wa Nigeria.

Kwa hakika katika kipindi kirefu cha kuendeshwa kesi ya Sheikh Zakzaky na mkewe, Saudia na utawala wa Kizayuni zimefanya juhudi kubwa ili apate kuhukumiwa na kupewa kifungo kirefu.

Duru mpya

Pamoja na hayo lakini sasa juhudi zote hizo zimegongwa mwamba kufuatia Mahakama Kuu ya Kaduna kufutilia mbali tuhuma zote bandia alizoelekezewa Sheikh pamoja na mke wake, na kuamuru wote waachiliwe huru mara moja. Tunatumai kuwa kufuatia kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky na kuanza duru mpya ya shughuli zake za Kiislamu, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria itapata moyo na msukumo mpya wa kuendesha shughuli zake kwa maslahi ya Waislamu wote wa Nigeria na hasa Mashia wa nchi hiyo.

 

3987241/

captcha