IQNA

Jinsi ya kuepuka israfu katika chakula

14:41 - November 14, 2021
Habari ID: 3474554
TEHRAN (IQNA)- Dini tukufu ya Kiislamu inawahimiza waumini kujiepusha na israfu hasa katika chakula kwani huku Waislamu wakiwa kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.

Mwenyezi Mungu SWT katika Qur'ani Tukufu sehemu ya aya ya 31 ya Sura Al' Araaf anasema:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ

"…na kuleni, na kunyweni na wala msifanye israfu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu."

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) huku mamilioni ya watu wakiwa hawana chakula na maelfu wakipoteza maisha kutokana na njaa kila mwaka. Kwa mfano ripoti ya  mwaka 2020/21 ya FAO karibu tani bilioni 1.3 za chakula hutupwa kila mwaka.

La kusikitisha ni kuwa, Saudi Arabia ambayo ni nchi ya Kiislamu inaongoza kati ya nchi 25 duniani zinazomwaga na kutupa jaani kiwango kikubwa zaidi cha chakula.

Kitengo cha wanataaluma wa masuala ya biashara cha jarida la The Economist, katika ripoti ya mwaka 2019 kilitangaza kuwa, kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi uliofanywa, nchi 25 zinamiliki karibu asilimia 87 ya Jumla ya Pato la Dunia na kwamba Wasaudia wanaongoza kati ya raia wa nchi zote duniani katika israfu ya umwagaji na utupaji mabaki ya chakula.

Wakati huo, Wizara ya Mazingira, Maji na Kilimo ya Saudia ilitangaza kuwa kila raia mmoja wa nchi hiyo humwaga kilogramu 250 za chakula kwa mwaka, kulinganisha na wastani wa dunia wa kilo 115. Kitengo cha Wanataaluma cha The Economist kinasisitiza kuwa, kiwango halisi cha utupaji chakula unaofanywa na kila raia mmoja wa nchi hiyo ni kikubwa zaidi ya kiwango hicho rasmi kilichotangazwa na serikali ya Riyadh. Kwa mujibu wa kitengo hicho, kiwango hicho ni karibu kilo 427 za chakula kwa mwaka.

Imeelezwa kuwa israfu hiyo ya umwagaji na utupaji chakula, mbali na kuisababishia Saudia hasara ya kiuchumi ya mabilioni ya dola kwa mwaka, inasababisha pia uharibifu wa mazingira na madhara ya kijamii.

Wakati nchi kadhaa za Kiarabu zinaongoza kwa israfu ya chakula, kwa mwaka wa saba sasa, wananchi wa nchi masikini zaidi ya Kiarabu ya Yemen wanaandamwa na hujuma na mashambulio ya kijeshi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia, ambayo mbali na kuteketeza roho za watu, yameisababishia nchi hiyo baa kubwa zaidi la njaa duniani. Aidha katika maeneo mengi duniani, mamilioni ya watu wakiwemo Waislamu hasa katika nchi za Afrika wanakumbwa na baa la njaa huku wengine wakiwa wamepoteza maisha.

Kupunguza upotevu na utupaji wa chakula ni muhimu katika dunia ambayo mamilioni ya watu wanalala njaa kila siku, limesema shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.  

Shirika hilo limesisitiza “Tunapopunguza utupaji chakula, tunaheshimu kuwa chakula hakipatikani kirahisi kwa mamilioni ya watu ambao wanalala njaa kila uchao. Ni juu yetu kubadili tabia zetu ili kufanya upotevu wa chakula kutokuwa ndio mfumo wa maisha maisha.” 

FAO imeainisha hatua rahisi ambazo kila mmoja anaweza kuchukua ili kukithamini na kukienzi chakula: 

  1. Tumia lishe bora na endelevu 

Maisha yanaenda kwa kasi na kuandaa chakula chenye lishe inaweza kuwa changamoto, lakini milo yenye afya si lazima itumie muda mrefu kuandaliwa. Mtandao umejaa mapishi ya haraka yenye afya ambayo unaweza kushiriki na familia yako na marafiki zako. 

  1. Nunua tu kile unachohitaji 

Panga chakula chako. Fanya orodha ya ununuzi na uizingatie, na epuka ununuzi wa kukurupuka. Sio tu utapoteza chakula kidogo, bali pia utaokoa pesa yako! 

  1. Chagua matunda na mboga zenye muonekano mbaya 

Usihukumu chakula kwa muonekano kwake. Matunda na mboga zenye umbo la kushangaza au zilizopondwa mara nyingi hutupiliwa mbali kwa sababu hazifikii viwango vya kupendezesha macho. Usijali kwani ladha ni ileile. Tumia matunda yaliyokomaa kwa kutengeneza urojo, juisi na kuyala jinsi yalivyo. 

4. Hifadhi chakula kwa busara 

Sogeza bidhaa za zamani mbele ya kabati yako au jokofu na mpya weka nyuma. Tumia vyombo visivyoingiza hewa kuweka chakula wazi kwenye jokofu na hakikisha vikasha vimefungwa ili kuzuia wadudu kuingia. 

5. Kuelewa uwekaji wa chakula hadi lini 

Kuna tofauti kubwa kati ya tarehe "bora kabla ya " (Best Before) na "matumizi ifikapo " (Use by or expiry date). Wakati mwingine chakula bado ni salama kula baada ya tarehe isemayo "bora kabla ya", lakini ni tarehe isemayo "matumizi ifikapo" ambayo inakuambia wakati gaani ni mwisho wa kutumia au sio salama tena kula.  

Angalia maandishi yanayoelezea kuhusu chakula hivyo kwa ajili ya  ya chakula vitu au viungo visivyofaa kwa afya kama vile mafuta na vihifadhi na epuka vyakula vilivyoengezwa sukari au chumvi. 

6. Anza kidogo 

Chukua sehemu ndogo nyumbani unapokula nyumbani  na ukiwa mgahawani gawana na wengine.

7.Penda mabaki yako 

Endapo hutoweza kula kila kitu, kihifadhi kilichosalia kwenye jokofu au fridge kwa ajili ya baadaye au tumia mabaki hayo kuandaa mlo mwingine. 

8. Geuza mabaki ya chakula kuwa mbolea 

Badala ya kutupa mabaki ya chakula chako, yatumie kama mbolea. Kwa njia hii unarudisha virutubishi kwenye mchanga na kupunguza kiwango cha uzalishaji wako wa hewa ukaa au hewa chafu. 

9. Heshimu chakula 

Chakula kinatuunganisha wote. Ungana tena na chakula kwa kujua mchakato wa kukiandaa. Soma juu ya uzalishaji wa chakula na uwajue wakulima wako. 

10. Saidia wakulima wa eneo lako 

Kwa kununua mazao ya ndani, unasaidia wakulima wa familia na wafanyabiashara ndogo ndogo katika jamii yako. Unasaidia pia kupambana na uchafuzi wa mazingira kwa kupunguza umbali wa kusafirisha chakula kwa malori na magari mengine. 

11. Kula samaki kwa wingi 

Kula zaidi aina mbalimbali za Samaki kama vile mackerel au sill, badala ya zile zilizo katika hatari ya kuvuliwa kupita kiasi, kama papa au jodari. Nunua samaki waliovuliwa au kufugwa kwa njia endelevu, kama samaki waliowekwa alama ya kujali mazingira au waliothibitishwa. 

12. Tumia maji kidogo 

Hatuwezi kuzalisha chakula bila maji. Ingawa ni muhimu kwamba wakulima watumie maji kidogo kukuza chakula, kupunguza taka ya chakula pia kunaokoa rasilimali zote za maji zilizoingia katika kuzalisha chakula.  

Punguza matumizi yako ya maji kwa njia zingine pia kama kukarabati mabomba yanayovuja au kufunga mabomba ya maji wakati unasafisha meno yako! 

13. Tunza udongo na maji 

Taka zingine za nyumbani zina hatari na hazipaswi kutupwa kwenye pipa la taka za kawaida. Vitu kama betri, rangi, simu za rununu, dawa, kemikali, mbolea, matairi, makasha ya wino, n.k zinaweza kuingia kwenye mchanga na mfumo wa usambazaji wa maji, na kuharibu rasilimali za asili zinazozalisha chakula chetu. 

14. Kula zaidi jamii ya kunde na mboga 

Mara moja kwa wiki, jaribu kula chakula cha jamii ya kunde au nafaka za kale kama vile quinoa. 

15. Gawia wenzako chakula

Changia na wengine chakula ambacho kingepotea bure. Kwa mfano, apu zinaweza kuwaunganisha majirani wao kwa wao na wafanyabiashara wa ndani ili chakula cha ziada kiweze kugawanywa, na sio kutupwa. 

1309609/

captcha