IQNA

Kesi ya kwanza ya COVID-19 aina ya Omicron yaripotiwa Saudia

20:36 - December 01, 2021
Habari ID: 3474627
TEHRAN (IQNA)- Saudi Arabia imeripoti kesi ya kwanza ya aina mpya ya COVID-19 ijulikanayo kama Omicron ambayo imegundulika katika raia wa nchi hiyo aliyerejea kutoka eneo la kaskazini mwa Afrika.

Aina hiyo ya COVID-19 ambayo iligunduliwa kwa mara ya kwanza na wanasayansi wa Afrika Kusini lakini uchunguzi zaidi umebaini kuwa ilikuwepo barani Ulaya kwa muda mrefu. Hivi sasa nchi nyingi duniani zimeanza kuweka vikwazo vya usafiri pamoja na kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema hatua kama hizo hazisaidii na zinaweza kuwa na madhara zaidi.

“Kesi ya COVID-19 aina ya Omicron imegunduliwa katika Ufalme na imepatikana baada ya kupimwa raia aliyewasili kutoka Afrika Kaskazini,” imesema taarifa ya Wizara ya Afya ya Ufalme wa Saudi Arabia.

“Amewekwa katika karantini pamoja na watu wote aliokutana nao na hatua za lazima zimechukuliwa,” imeongeza taarifa hiyo. Hii ndio kesi ya kwanza ya Omicron katika eneo zima la Ghuba ya Uajemi.

Saudi Arabia wiki iliyopita ilisitisha safari za ndege kutoka nchi sita za kusini mwa Afrika baada ya kuibuka aina hiyo mpya ya corona.

Katika wiki za hivi karibuni Saudia imetangaza kuondoa vikwazo vilivyowekwa kwa waumini wa dini ya Kiislamu wanaotaka kutembelea maeneo matakatifu ya Makka na Madina ambapo hivi sasa raia wa kigeni wanaruhusiwa kutekeleza Hija ndogo ya Umrah kwa sharti la kuwa wamechanjwa na wamepimwa korona kabla ya kuingia katika ufalme huo.

Hadi sasa watu 549,000 wameambukizwa COVID-19 ambapo 8,836 miongoni mwao wamefariki dunia.

3476749

captcha