IQNA

Hamas yaipongeza Malaysia kwa misimamo dhidi ya Wazayuni

20:08 - December 02, 2021
Habari ID: 3474629
TEHRAN (IQNA) – Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeipongeza Malaysia kwa msimamo wake wa kupinga kuanzisha uhusiano na adui Mzayuni.

Katika taarifa Jumatano, Hamas imeipongeza Malaysia kwa kukataa kutoa visa kwa wanariadha wa utawala wa Kizayuni wa Israel jambo ambalo lilipelekea Mashindano ya Kimataifa ya Squash yaliyopangwa kufanyika nchini humo kufutwa kutokana na msimamo huo wa Malaysia. Shirikisho la Kimataifa la Squash limefuta mashindano hayo ya Malaysia kwa sababu wanariadha hao wa utawala haramu wa Israel hawakupata visa. Hamas imesema uamuzi wa shirikisho hilo ni ishara ya kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hamas imetangaza mshikamano na Malaysia kutokana na msimamo wake katika mashindano hayo yaliyofutwa na mashindano mengine ya kimataifa.

Taarifa ya Hamas imesema utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kukalia kwa mabavu na kuzikoloni ardhi za Palestina mbali na kutenda kila aina ya jinai dhidi ya Wapalestina ikiwa ni pamoja na kuharibu kabisa sekta ya michezo ya Wapalestina. Hamas imesema kwa kuzingatia jinai hizo, Israel haipaswi kushiriki katika mashindano ya kimataifa.

Mashindano Ya Kimataifa ya Squash yalikuwa yafanyike Disemba 7-12 mjini Kuala Lumpur lakini Shirikisho la Kimataifa la Squash limetangaza kufuta mashindano hayo baada ya wanariadha hao wa Israel kunyimwa visa ya kuingia katika nchi hiyo.

3476757

captcha