IQNA

Utawala wa Israel wabomoa kituo cha afya mjini al-Quds

17:22 - January 04, 2022
Habari ID: 3474766
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa Kizayuni wa Israel umebomoa kituo cha afya na majengo mengine kadhaa katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Duru za habari Palestina zinadokeza kuwa, askari wa utawala wa Israel wakiwa katika magari ya deraya walivamia kijiji cha Jabel al Mukaber kusini mashariki mwa Quds ambapo walisimamia mabuldoza ambayo yalibomoa Kituo cha Afya cha Abdullah al Sheikh.

Aidha mabuldoza hayo ya utawala wa Israel yalibomoa jengo jingine katika eneo la Beit Hanina kaskazini mwa mji wa Quds.

Halikadhalika Jumanne magari ya jeshi la Israel yalivamia kijiji cha Al Zaeem mashariki mwa mji wa Quds na kuharibu mashamba ya Wapalestina.

Utawala dhalimu wa Israel mara kwa mara hubomoa nyumba za Wapalestina kwa visingizio mbali mbali kwa lengo la kuwapa makazi haramu walowezi wa Kizayuni.

Utawala haramu wa Israel ulikalia kwa mabavu ardhi za magharibi mwa mji mtakatifu wa Quds ambazo zinajumuisha Msikiti wa al-Aqsa ambao ni msikiti wa tatu kwa utukufu katika ulimwengu wa Kiislamu mwaka 1948. Mwaka 1967 ulikalia kimabavu ardhi zaidi za mashariki ambazo Malaka ya Ndani ya Palestina imedhamiria kuzifanya kuwa mji mkuu wake.

Licha ya kuwa jamii ya kimataifa inazochukulia ardhi hizo kuwa zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa kibaguzi wa Israel lakini haijachukua hatua zozote za maana za kuulazimisha utawala huo uwarudishie Wapalestina ardhi zao hizo.

Desemba 23, 2016 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio 2334 ambalo liliutaka utawala haramu wa Israel usimamishe haraka na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kwa kuyazayunisha maeneo hayo, kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.

Karibu jamii nzima ya kimataifa inasisitiza kuwa hatua ya Israel kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi ni kinyume cha sheria.

3477229

captcha