IQNA

Inna Lillah wa Ina Ilayhi Rajioun

Sheikh Abdillahi Nassir, msomi mkubwa wa Kiislamu Afrika ameaga dunia

12:34 - January 11, 2022
Habari ID: 3474792
TEHRAN (IQNA)- Sheikh Abdillahi Nassir Juma Bhalo, msomi maarufu wa Kiislamu barani Afrika na hasa Afrika Mashariki ameaga dunia mapema leo Mombasa, Kenya.

Umma wa Kiislamu umetumbikia katika majonzi makubwa kufuatia kuaga dunia Sheikh Abdillahi Nassir, ambaye alitumia umri wake wote uliojaa baraka kuwatumiakia Waislamu na taifa zima la Kenya kwa ujumla.

Sheikh Abdillahi Nassir alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Ahul Bayt wa Mtume Muhammad SAW na alipata umaarufu kama mwanazuoni, mwalimu, mhadhiri na mwandishi maarufu wa Kiislamu mbali na kuwa miongoni mwa wajumbe wa  Kenya katika mazungumzo ya kupigania uhuru ya Lancaster huko London mwaka 1960

Marehemu alikuwa mwanachuoni mcha Mungu,mvumilivu, mnyenyekevu na mpambanaji katika njia ya Mwenyezi Mungu na hakuacha kushauri, kutoa muongozo na maelekezo hadi mwisho wa uhai wake.

Sheikh Abdillahi Nassir aliandika vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, vilivyosaidia pakubwa kujenga na kukuza imani za Waislamu.

Katika miaka ya karibuni amekuwa akijishughulisha na uandishi wa tafsiri ya Qur’ani Tukufu kwa lugha ya Kiswahili na kueneza mafundisho ya Ahlul Bayyt AS. Miongoni mwa vitabu vya marehemu Sheikh Abdillahi Nassir ni Shia na Qur'ani, Maulidi si Bidaa, Si Haramu, Ukweli wa Hadithi ya Kisaa, Mut'a Ndoa Halali, Ukweli wa Hadithi ya Karatasi, Ahlul Bayt Ni Nani? na Yazid Hakuwa Amirul Muuminin.

Shirika la Habari la IQNA linachukua fursa hii kutuma salamu za rambi rambi kwa Imam wa Zama, familia ya marhum Sheikh Abdillahi Nassir,  wanafunzi wake, na Waislamu wote kwa ujumla na tunamuomba Mwenyezi Mungu amrehemu na amsamehe dhambi zake na amlipe ujira mkubwa kwa huduma zake kwa Uislamu. 

4027807

captcha