IQNA

Rais wa Iran katika mazungumzo na Rais wa Ufaransa

Mapatano ya Vienna lazima yajumuishe kuondoelwa vikwazo vyote

17:51 - February 20, 2022
Habari ID: 3474953
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mapatano yoyote yatakayofikiwa kwenye mazungumzo ya Vienna yenye lengo la kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA lazima yajumuishe suala la kuondolewa vikwazo taifa la Iran, sanjari na kupasishwa kwa kipengee kuhusu dhamana yenye itibari, na vile vile kujizuia na masuala ya kisiasa na kuibua tuhuma zisizo na msingi.

Rais Raisi alisema hayo jana Jumamosi katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron na kusisitiza kuwa, ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo hayo umejitolea kwa dhati ili kuona tija inafikiwa.

Sayyid Raisi ameashiria maendeleo yaliyopatikana kufikia sasa kutokana na mapendekezo mazuri ya Iran na kubainisha kuwa, Iran inataka dhamana ya kutokiukwa tena makubaliano hayo, kwani hiyo ni haki ya msingi ya wananchi wa Iran.

Amesema historia ya uhusiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) imethibitisha kuwa miradi ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu yana na malengo ya amani na kiraia, na kwamba baadhi ya mataifa yanapaswa kujiepusha kutoa madai yasiyo na msingi juu ya miradi hiyo.

Awamu ya nane ya mazungumzo ya Vienna ambayo maudhui yake ni kuondolewa vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa Iran, iliendelea tena Jumanne ya Februari 8, 2022, baada ya kusimama kwa muda mfupi ili kutoa fursa kwa timu za mazungumzo kurejea katika nchi zao kwa mashauriano zaidi.

Awamu hiyo imeshuhudia maendeleo mazuri kutokana na mapendekezo mazuri ya Iran. Hata hivyo nchi za Magharibi ikiwemo serikali ya Joe Biden huko Marekani inaendelea kutekeleza vikwazo vya utawala uliopita wa nchi hiyo na hadi sasa nchi hizo za Ulaya na Marekani ndizo zinazozorotesha kufikiwa makubaliano ya mwisho huko Vienna.

Kwa upande wake, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema hatua nzuri zimepigwa kufikia sasa kwenye mazungumzo hayo ya Vienna, na wanatumai yatafikia tamati haraka iwezekanavyo.

/4037453

captcha