IQNA

Mashindano ya kimataifa ya wanafunzi wa shule kufanyika Iran

8:01 - February 27, 2022
Habari ID: 3474981
TEHRAN (IQNA)- Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Qur'ani, Itra na Sala cha Wizara ya Elimu na Malezi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vijana wadogo 20 wameingia kwenye fainali ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu kwa wanafunzi wa shule za Ulimwengu wa Kiislamu.

Mikaeel Bagheri amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, Mashindano ya Saba ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu kwa wanafunzi wa shule za Ulimwengu wa Kiislamu mwaka huu yamekuwa na vijana 20 walioingia fainali, 12 wavulana na nane wasichana. Mashindano hayo yanafanyika katika fani za hifdh na qiraa.

Amesema, kati ya wanafunzi hao 20 walioingia fainali, 6 ni maqarii wanaume, wanne maqarii wanawake, 6 wanafunzi wa kiume wa fani ya hifdh na wanne wanawake fani ya hifdh. 

Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Qur'ani, Itra na Sala cha Wizara ya Elimu na Malezi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema: Mwaka huu wanafunzi 50 wa nchi 25 tofauti za Ulimwengu wa Kiislamu walifanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano hayo.

Fainali za Mashindano hayo ya Saba ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu kwa wanafunzi wa skuli za Ulimwengu wa Kiislamu zimepangwa kufanyika kuanzia tarehe tarehe 27 Rajab hadi tarehe 2 Shaaban 1443 Hijria, zitakazosadifiana na tarehe  Mosi Machi hadi 5 Machi mwaka huu wa 2022. Fainali hizo zitafanyika kwa mnasaba wa maadhimisho ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW katika hoteli ya Laleh, jijini Tehran. Iran ni nchi pekee duniani inayoandaa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani maalumu kwa wanafunzi wa shule.

3477967

captcha