IQNA

Waislamu Japan wakabiliwa na changamoto za maeneo ya kuzika

12:48 - May 12, 2022
Habari ID: 3475239
TEHRAN (IQNA)-Ingawa idadi ya Waislamu wa Japani inaendelea kuongezeka, kuna makaburi machache sana katika nchi hii, ambapo kuchoma maiti ni jambo la kawaida.

Takriban Waislamu 230,000 walikuwa wakiishi Japani kufikia mwisho wa 2020, kulingana na Hirofumi Tanada, profesa wa sosholojia katika Chuo Kikuu cha Waseda. Idadi hiyo inatabiriwa kuongezeka kila mwaka.

Pamoja na hayo ni makaburi saba tu nchini Japani yanakubali mazishi ya Waislamu.

Kwa mfano Kanda nzima ya Kyushu haina makaburi ya Waislamu licha ya juhudi za muda mrefu za Jumuiya ya Waislamu wa Beppu huko Beppu, Mkoa wa Oita.

Jumuiya hiyo inapanga kufungua makaburi ya mazishi ya Waislamu katika jiji hilo mashuhuri kwa utalii  lakini wakazi wa eneo hilo walipinga.

Kisha kundi hilo liliwasilisha ombi kwa wizara ya afya mwezi Juni mwaka jana, wakiiomba ifungue “makaburi ya kitamaduni,” ambapo watu wanaweza kuzikwa kwa kuzingatia dini zao au kwa sababu nyinginezo.

"Kwa Waislamu, kuchoma maiti ni kutoheshimu wafu," alisema Khan Muhammad Tahir, mkuu wa jumuiya hiyo na profesa wa uhandisi wa mtandao wa mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Ritsumeikan Asia Pasikifiki. "Wazo la kuchoma maiti ni chungu zaidi na lenye kuhuzunisha."

Tahir alisema Waislamu wanakabiliwa na matatizo makubwa ikiwa hakuna makaburi ya ndani ya nchi ambayo yatakubali kuzikwa kwao.

Alisema kuwa kusafirisha miili hadi maeneo ya mbali nchini Japani au hata nje ya nchi ni jambo gumu na la gharama kubwa.

Waislamu wengi wameishi Japan kwa miongo kadhaa na wana makazi kamili nchini humo.

Moja ya Makaburi ya Japan yanayokubali Mazishi ya Waislamu ni Makaburi ya Hanya Kodama Seichi Rain (Makaburi ya Hanya Kodama) huko Hanya, Mkoa wa Saitam.

Waisalmu 42 wamezikwa katika Makaburi hayo na katika aghalabu ya kila kaburi kuna maandishi ya Kiarabu. Makaburi mengine ni vilima tu bila mawe ya kaburi.

Makaburi hayo yalianza kukubali kuzikwa kwa Waislamu mnamo Juni 2019. Mwislamu wa kwanza kuzikwa hapa alikuwa Mghana aliyeishi Soka, Mkoa wa Saitama.

Tangu wakati huo, Waislamu wa mataifa mbalimbali wamezikwa katika makaburi hayo, kwa mujibu wa kumbukumbu zake. Wanajumuisha Wapakistani, Wabangladeshi, Wasri Lanka, Wairani, Waafrika Kusini, Wachina, Wasaudi, na Waindonesia.

Rekodi hizo pia zilionyesha jina la mwanamke wa Kijapani, ambaye pengine aliolewa na mwanamume Mwislamu.

3478865

Kishikizo: japan waislamu
captcha