IQNA

Ukandamizaji

Saudia yaidhinisha hukumu ya kunyongwa vijana wawili wa Kishia

22:39 - May 21, 2022
Habari ID: 3475275
TEHRAN (IQNA)- Mahakama ya Juu ya Saudia imeendeleza sera za kuwaua Waislamu wa madhehebu ya Shia kwa kuidhinisha hukumu ya kuwanyonga vijana wawili raia wa Bahrain.

Kwa muda sasa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia umeshadidisha utekelezaji wa hukumu za kuwanyonga Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Kwa mujibu wa jarida la Saut al Manama, Mahakama ya Juu ya Saudi Arabia hivi karibuni iliwatuhumu vijana wawili wa Bahrain kuwa walikuwa wakilenga kutekeleza opareheni za uharibifu ndani ya ardhi ya Saudia. Hata hivyo hakuna ushahidi wala nyaraka zozote zinazothibitisha kuwa vijana hao wana hatia.

Kufuatia hukumu hiyo, Muungano wa 'Vijana wa Februari 14' nchini Bahrain umelaani vikali hukumu hiyo ya Mahakama ya Juu ya Saudia na kutangaza kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kuzuia sera hizo haribifu za Saudia.

Muungano huo umeongeza kuwa, hatua zinapaswa kuchukuliwa kuzuia utekelezaji wa hukumu ya kunyongwa Sadiq Thamr na Jaafar Sultan. Kwa kutolewa hukumu hiyo ya Mahakama ya Juu ya Saudia, yamkini vijana hao wakanyongwa wakati wowote ule.

Hadi sasa Saudia imewanyonga makumi ya wakaazi wa eneo lenye Mashia wengi la Qatif. Siku chache zilizopita, raia wawili Mashia wa Saudia walinyongwa. 

Wananchi wa mashariki mwa Saudi Arabia wamekuwa wakiandamana mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni wakilalamikia vitendo vya ukandamizaji vya utawala wa Saudia na mauaji ya makumi ya waandamanaji katika miji ya Al-Awamiyah na Qatif, lakini kila mara wamekuwa wakikandamizwa vikali na kuuliwa na vikosi vya Al-Saud.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa, Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa kunyonga wapinzani wa kisiasa na imekuwa ikilaumiwa sana kutokana na rekodi yake mbaya ya kukanyaga haki za binadamu.

4058403

captcha