IQNA

Mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel

Radiamali baada ya Bunge la Iraq kutangaza uhusiano wowote na Israel ni uhalifu

17:15 - May 28, 2022
Habari ID: 3475306
TEHRAN (IQNA)- Alkhamisi tarehe 26 Mei, 2022, Bunge la Iraq lilipasisha kwa kauli moja sheria ya kutambua kuwa ni uhalifu, hatua yoyote ya kuweka uhusiano wa kawaida baina ya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Muswada huo uliwasilishwa bungeni na mrengo wa Sadr unaoongozwa na Muqtada al Sadr. Kwa sheria hiyo, Bunge la Iraq limepiga marufuku uhusiano wa aina yoyote ile wa kisiasa, kiusalama, kiuchumi, kiufundi, kielimu na kimichezo na utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheria hiyo imetamka wazi kuwa marufuku hiyo inawahusu raia wote wa Iraq wa ndani na nje ya nchi hiyo wakiwemo viongozi na wafanyakazi wa serikali pamoja na maafisa wa kijeshi na raia wa kawaida, watu wa huduma za uma na mgeni yeyote aliyemo ndani ya Iraq. Aidha marufuku hiyo inahusu asasi zote za kiraia na za kiserikali, serikali za kieneo na mabunge pamoja na idara zao na vyombo vya habari vya Iraq, mitandao ya kijamii, na pia mashirika binafsi na ya kigeni yaliyo na vitega uchumi na yanayofanya kazi ndani ya Iraq.

Kiujumla ni kwamba sheria hiyo inawahusu hata raia wasio wa Iraq ambao wako nchini humo kwa shughuli yoyote ile. Wote hawana haki wa kuwa na ushirikiano wowote na utawala wa Kizayuni wa Israel ndani ya ardhi ya Iraq. Nukta nyingine muhimu ni kwamba kwa mujibu wa sheria hiyo, adhabu ya kifo itatolewa kwa mtu yeyote ambaye atakhalifu sheria hiyo. Kipengee hicho kinaonesha umuhimu mkubwa wa sheria hiyo na jinsi Bunge la Iraq lilivyokusudia kikwelikweli kupambana na uhusiano wa aina yoyote ile na utawala pandikizi wa Israel.

Wabunge wa Iraq wapongezwa

Mara baada ya kupasishwa sheria hiyo, Wabunge walipaza sauti wakipiga nara dhidi ya utawala haramu wa Israel. Wananchi na shakhsia mbalimbali wa Iraq wamelipongeza Bunge la Iraq kwa hatua hiyo, huku harakati za mapambano huko Palestina na Lebanon nazo zikisifu uamuzi huo ambao ni uungaji mkono wa wazi kwa taifa madhulumu la Palestina linalokandamizwa na Wazayuni maghasibu. 

Wakati huo huo Kamati ya Uratibu ya Waislamu wa Kishia nchini Iraq imetoa tamko rasmi na kutangaza kuwa, Bunge la nchi hiyo limethibitisha kivitendo kwamba halitetereki hata kidogo katika msimamo wake wa kimsingi wa kulihami na kuliunga mkono taifa la Palestina na kadhia ya Quds. Kamati hiyo imeongeza kuwa, hatua ya Bunge la Iraq ya kupasisha sheria ya kupiga marufuku uhusiano wa kiwango na aina yoyote na utawala wa Kizayuni wa Israel inaonesha jinsi Wairaq wote walivyo na msimamo mmoja kuhusu masuala ya kitaifa na Kiislamu.

Siku ya Bendera

Hatua hiyo ya Bunge la Iraq imechukuliwa wakati huu wa kukaribia kufanyika "Maandamano ya Siku ya Bendera" ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika kesho Jumapili, Mei 29, 2022. Lakini Wapalestina kwa umoja wao, wote wanapinga vikali maandamano ya kuadhimisha siku hiyo. Bila ya shaka yoyote hatua ya Bunge la Iraq ya kupasisha sheria kali ya kupiga marufuku kikamilfu uhusiano wa kiwango na aina yoyote na utawala wa Kizayuni, ni kutangaza wazi wazi uungaji mkono wa taifa la Iraq kwa ndugu zao Wapalestina. Lakini pia hatua hiyo ya Bunge la Iraq ni tangazo la wazi la hasira za Wairaq wote dhidi ya jinai na ukatili unaondelea kufanywa na Israel huko Palestina.

Usaliti wa tawala za Kiarabu

Nukta ya mwisho tunayopenda kuigusia hapa ni kwamba, ijapokuwa nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain, Sudan na Morocco zimejidhalilisha na kuwasaliti Waislamu na Wapalestina kwa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, na hata kama Saudi Arabia nayo imeongeza sana ushirikiano wake na utawala huo dhalimu, katili na pandikizi, lakini hatua ya bunge la Iraq ya kupiga marufuku uhushiano na ushirikiano wa aina yoyote na utawala pandikizi wa Israel ni uthibitisho kuwa wananchi na mataifa ya Kiarabu hayafurahishwi hata kidogo na kitendo cha viongozi wa nchi hizo nne za Kiarabu cha kujidhalilisha mbele ya Wazayuni na kwamba jinamizi la kutengwa bado linauandama utawala wa Kizayuni hasa kutoka kwa nchi kubwa na zenye idadi kubwa ya watu za Ulimwengu wa Kiarabu.

4060033

captcha