IQNA

Kiongozi Muadhamu katika mkutano na Rais Maduro wa Venezuela

Uzoefu umeonyesha mapambano ndio njia pekee ya kukabiliana na mashinikizo ya Marekani

11:42 - June 12, 2022
Habari ID: 3475366
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema uzoefu wenye mafanikio wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Venezuela katika kupambana na vikwazo vya Marekani umedhihirisha wazi kuwa, mapambano au muqawama ndio njia pekee ya kuzima mashinikizo ya namna hiyo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema hayo jana jioni hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro ambaye aliwasili hapa Tehran juzi Ijumaa kwa ziara rasmi ya siku mbili.

Ayatullah Khamenei amempongeza Rais Maduro na taifa la Venezuela kwa jumla kwa kusimama kidete mkabala wa mashinikizo ya Washington na kusisitiza kuwa: Hii leo, mtazamo wa Marekani kwa Venezuela ni tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Ameeleza bayana kuwa, "mapambano yako na ya wananchi wa Venezuela yana thamani kubwa kwa kuwa yanaimarisha thamani na hadhi ya taifa, nchi na viongozi wake."

Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mafanikio ya Iran katika nyuga za sayansi na teknolojia na kueleza kuwa, hatua hizo zilipigwa wakati ambapo taifa hili lilikuwa chini ya vikwazo shadidi vya Marekani vilivyoitwa 'mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi.'

Aidha Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amepongeza hatua ya Iran na Venezuela kusaini makubaliano ya ushirikiano ya miaka 20, katika nyuga za sayansi, teknolojia, kilimo, mafuta na gesi, petrokemikali, utalii na vilevile utamaduni na kusisitizia haja ya kutekelezwa mapatano hayo kwa muda mrefu.

Hali kadhalika, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza msimamo Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kubainisha kuwa, 'msimamo huo ni wa dhati, sahihi na wa kishujaa."

Kwa upande wake, Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro mbali na kusisitizia haja kuimarishwa zaidi uhusiano wa Caracas na Tehran katika nyuga tofauti hususan ulinzi, uchumi na nishati, ametangaza pia uungaji mkono wake kwa wananchi wa Palestina na kueleza kuwa, Tel Aviv imekuwa ikila njama nyingi chafu dhidi ya Caracas, kupitia shirika la ujasusi la Israel Mossad. 

4063557

captcha