IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /23

Surah Al-Mu’minun: Waumini wa Kweli Ni Wapi?

18:16 - August 03, 2022
Habari ID: 3475575
TEHRAN (IQNA) – Surah Al-Mu’minun ni sura ya Makki ya Qur’ani Tukufu inayoeleza sifa za waumini wa kweli.

Sura ya 23 ya Qur'ani Tukufu ina aya 118 na iko katika Juzuu 18 ya Kitabu kitukufu. Ni Sura ya 74 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume (SAW).

Jina lake ni Al-Mu’minun (waaminifu, waumini) kwa sababu inarejelea wokovu wa waaminifu katika aya yake ya kwanza (Wamefanikiwa Waumini), na kisha inaeleza 15 ya sifa zao.

Kuwatahadharisha waumini kujiepusha na maneno ya upuuzi, kuwahimiza watoe sadaka na wafanye matendo mema, kuashiria hadithi za Nabii Nuh (AS) na Nabii Musa (AS), kuumbwa kwa mwanadamu na Siku ya Kiyama ni miongoni mwa maudhui nyingine katika sura hii.

Katika Tafsiri yake ya  Al-Mizan ya Qur'ani Tukufu, Allameh Tabatabaei anasema imani kwa Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama, kubainisha tabia za waumini na maovu ya kimaadili ya makafiri, bishara njema na maonyo yanayotolewa kwa waumini na makafiri, na adhabu wanazopewa, watu wa zamani ni miongoni mwa mada kuu za Sura.

Yaliyomo katika Surah Al-Mu’minun yanaweza kugawanywa katika kategoria saba:

Sehemu ya kwanza inayoanza na aya za kwanza inafafanua sifa zinazowasaidia waumini kufanikiwa, sifa zinazohusu nyanja zote za maisha yao.

Katika sehemu ya pili, ishara tofauti za Mwenyezi Mungu na mifano ya ulimwengu wa ajabu wa uumbaji duniani na angani pamoja na uumbaji wa wanadamu, wanyama na mimea imetajwa.

Sehemu ya tatu inasimulia hadithi za idadi kubwa ya manabii wakubwa kama Nuh (AS), Hud (AS), Musa (AS), na Isa au Yesu (AS), ikiashiria baadhi ya matukio katika maisha yao.

Katika sehemu ya nne, madhalimu na wakandamizaji wanaonywa kwa sababu za kimantiki na wakati mwingine kwa maonyo makubwa ya kubadili njia yao ili warejee kwa Mwenyezi Mungu.

Sehemu ya tano ina mjadala mfupi juu ya Siku ya Kiyama na katika sehemu ya sita, Sura inazungumzia utawala wa Mwenyezi Mungu juu ya ulimwengu na jinsi amri yake inavyotawala juu ya ulimwengu wote.

Na katika sehemu ya saba inazungumzia tena Siku ya Kiyama, hukumu na tathmini ya matendo, na malipo kwa watu wema na adhabu kwa madhalimu.

Sura inamalizia kwa kutambulisha lengo la uumbaji. Kwa ujumla, Sura inatoa mfululizo wa mafunzo juu ya imani na masuala ya kivitendo na inaonyesha njia ya waumini kutoka mwanzo hadi mwisho.

Habari zinazohusiana
captcha