IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Iran yalaani vikali kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu Ujerumani

12:19 - August 08, 2022
Habari ID: 3475593
TEHRAN (IQNA)- Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali kitendo cha kichochezi cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu, na kutusiwa matukufu ya Kiislamu nchini Ujerumani.

Nasser Kanaani Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuvunjiwa heshima matukufu hayo ya Kiislamu ni mfano wazi wa vitendo vya uhaini vinavyoeneza chuki, na vinavyolaaniwa na Waislamu wote, wafuasi wa dini zinazomuamini Mungu Mmoja, na wapenda haki, amani na mazungumzo miongoni mwa watu wa dini tofauti.

Huku akionya kuhusu matokeo mabaya ya vitendo hivyo vya kifasiki, Kanaani amebainisha kuwa, kitendo chochote cha kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu, ni sehemu ya misimamo ya kuchupa mipaka na yenye misingi ya fikra za matakfiri na magaidi wa Daesh (ISIS).

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema serikali zinazodai kuwa zinatetea haki za binadamu, uhuru na demokrasia zina wajibu wa kuweka mikakati na hatua za kuzuia vitendo vya aina hii. 

Vitendo hivyo vichafu vya kukinajisi Kitabu Kitukufu cha Waislamu na kuyatukana matukufu ya Kiislamu vilifanyika jana Jumapili nje ya Kituo cha Kiislamu cha Hamburg nchini Ujerumani.

Mwezi Juni mwaka huu, shirika moja la kutetea haki za binadamu nchini Ujerumani liliripoti kuwa limesajili matukio zaidi ya 800 ya kushambuliwa misikiti na maeneo matakatifu ya Waislamu nchini humo.

Hayo yamejiri katika hali ambayo, Waislamu barani Ulaya hadi sasa wameshabainisha mara kadhaa hofu na wasiwasi mkubwa walionao kuhusiana na hatua za chuki dhidi ya Uislamu pamoja na hujuma na mashambulio dhidi ya misikiti na vituo vya Kiislamu katika nchi za bara hilo na kutaka hatua kali zaidi za ulinzi na usalama zichukuliwe kwa ajili ya kuyalinda maeneo hayo.

3480010

captcha