IQNA

Kadhia ya al-Quds

Uingereza yatakiwa kutohamishia Ubalozi wake mjini Al-Quds

19:50 - October 01, 2022
Habari ID: 3475863
TEHRAN (IQNA) - Wajumbe wote wa nchi za Kiarabu nchini Uingereza wameripotiwa kutoa wito kwa nchi hiyo kutohamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Al-Qud (Jerusalem) .

Wamemwandikia barua Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss wakimtaka asiendelee na mpango huo ambao wameutaja kuwa “mbaya".

Mabalozi hao wa nchi zake Kiarabu walisema kuwa mpango huo unaweza kuhatarisha mazungumzo kuhusu makubaliano ya biashara huria kati ya Uingereza na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi yanayotarajiwa kukamilika mwaka huu.

Ripoti hiyo ilisema kwamba ingawa ilitarajiwa kwamba nchi kadhaa za Kiarabu zitapinga hatua hiyo, barua hiyo ina uthibitisho wa "nchi zote za Kiarabu," zikiwemo zile zinazounga mkono makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waliotia saini barua hiyo ni pamoja na UAE na Bahrain, nchi mbili za kwanza za Kiarabu ambazo zilianzisha uhusiano wa kawaida na Israeli mnamo 2020.

Truss ametangaza katika barua kwa jumuiya ya Conservative Friends of Israel yaani Wahafidhina Marafiki wa Israel  kwamba anatafakari  kuhamishia Jerusalem  ubalozi wa Uingereza ulioko TelAviv. Pia alimwambia waziri mkuu wa Israel Yair Lapid mjini New York wiki iliyopita kwamba ofisi yake inashughulikia suala hilo la kuhamisha ubalozi huo.

Husam Zomlot, balozi wa Palestina huko London, alisema hatua yoyote ya kuhamisia al-Quds ubalozi wa Uingereza itakuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na majukumu ya kihistoria ya Uingereza.

Israel inaidai umiliki wa al Quds nzima, lakini jumuiya ya kimataifa inaiona sekta ya mashariki ya mji huo kama eneo linalokaliwa kwa mabavu na Wapalestina wanaiona kuwa mji mkuu wa taifa lao la baadaye.

Mwezi uliopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina ilisema utawala wa Kizayuni wa Israel hauna madai wala mamlaka yoyote juu ya al Quds inayokaliwa kwa mabavu na kuongeza kuwa, hatua  ya Uingereza kuhusu ubalozi itakuwa sawa na "kushirikiana na Israel katika kuuteka mji huo kinyume cha sheria.”

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya  Palestina Hamas pia imesema kuhamishwa kwa ubalozi wa Uingereza hakutaupa uhalali wowote utawala wa Israel.

"Tangazo la Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss kuhusu nia yake ya kuhamisha ubalozi wa nchi yake kwenda al-Quds ni upendeleo wa wazi kwa utawala unaoukalia kwa mabavu mji huo," msemaji wa Hamas Abdel Latif Qanou alisema.

3480691

captcha