IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu Ufaransa

Ufaransa yalenga kuibua Waislamu bila Uislamu huku misikiti ikiendelea kufungwa

19:18 - October 04, 2022
Habari ID: 3475877
TEHRAN (IQNA) - Serikali ya Ufaransa imefunga makumi ya misikiti katika kipindi cha miaka miwili hivi kwa kisingizio cha sheria yenye utata na iliyokosolewa sana.

Ufaransa imeanza harakati za kuufunga msikiti wa Obernai katika eneo la Bas-Rhin. Lakini hii si mara ya kwanza kufanya hivyo.

Tangu 2020, kumeripotiwa kufungwa kwa misikiti 23 kote Ufaransa, katika kile wakosoaji wanasema ni hatua ya moja kwa moja dhidi ya Waislamu wa Ufaransa, ambao ni asilimia sita ya jumla ya watu wote.

Waziri wa Mambo ya Ndani na Nje wa Ufaransa Gerald Darmanin alifichua hayo kwenye mtandao wake wa Twitter, akisema, "Kwa ombi la Rais wa Jamhuri, mapambano dhidi ya harakati ya Kiislamu ya kutaka 'kujitenga' yanaendelea. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, maeneo 23 ya ibada yaliyojitenga yamefungwa."

Hisia hizi zinazoongezeka dhidi ya Uislamu katika wigo wa kisiasa wa Ufaransa zimekuwa sababu ya wasiwasi kwa wanaharakati wa haki za binadamu na mashirika ya kutetea haki.

Katika takriban matukio yote ya kufungwa kwa misikiti, wawakilishi wa misikiti hiyo wanasema serikali ya Ufaransa imetoa ushahidi usio wa kutosha kuhusu misingi ya maamuzi yao.

Serikali ya Ufaransa sasa ina uwezo mkubwa iliojitwika na wanaharakati wa haki, mashirika ya kimataifa - ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa - na wanachama wa jumuiya ya Waislamu wanasema uwezo huo huwapa maafisa wa serikali mamlaka mutalki ya kufunga maeneo ya ibada bila uchunguzi wa kutosha.

Fionnuala Ni Aolain, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi wa haki za binadamu wakati akikabiliana na ugaidi amewaambia waandishi habari kuwa mfumo unaotumika kuwakandamiza Waislamu wa Ufaransa ni wa kiimla.

Ripoti mpya iliyotolewa hivi karibuni ya kuhusu Chuki Dhidi ya Uislamu Barani  Ulaya 2021, inataja katika muhtasari wake wa utendaji wa hali ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa na kubaini kwamba "sheria hii, ambayo inapaswa kutoa jibu kali dhidi ya 'ugaidi' imechochea ukandamizaji mkali juu ya kuonekana kwa wenye utambulisho dhahiri wa Kiislamu

"Inaathiri kwanza Waislamu wanaoonekana zaidi kwa kupanua marufuku ya alama za kidini kwenye maeneo mengine mengi na inaharamisha jaribio lolote la kuandaa ibada huru ya Kiislamu..."

Moja ya matokeo muhimu katika ripoti hiyo inasema kwamba kufungwa au kuvunjwa kiholela kwa mashirika mengi ya Kiislamu kama vile vyama, shule, misikiti, migahawa au nyumba za uchapishaji mara nyingi kumethibitishwa kwa sababu zisizo na mashiko.

"Pia ni muhimu kuhoji nia ya serikali ya Ufaransa katika kutekeleza sera ambayo inafikia hatua ya kuharamisha Uislamu," ripoti hiyo inasema.

"Chuki dhidi ya Uislamu auIslamophobia nchini Ufaransa kimsingi ni matokeo ya serikali, ambayo inataka kuanzisha 'Uislamu wa Kifaransa' ambao unaondoa hali ya kujiamulia mambo Waislamu wa Ufaransa na kuwafanya 'Waislamu bila Uislamu'."

3480716

captcha