Marjaa na kiongozi mkuu wa kidini wa Lebanon Allamah Muhammad Hussein Fadhlullah ameitaka Jumuiya ya Maualama wa Kiislamu Duniani kujali zaidi umoja wa Waislamu hususan katika kukabiliana na changamoto, tuhuma mbalimbali zinazotolewa dhidi ya dini hiyo na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Kiislamu.
Ofisi ya IQNA nchini Lebanon imeripoti kuwa Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah aliyasema hayo katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu Duniani Salim al Awwa mjini Beirut. Amesema kuwa jumuiya hiyo iliundwa kwa lengo la kuwaunganisha Waislamu kupitia njia ya mazungumzo kati ya madhehebu mbalimbali za Kiislamu na kuchunguza njia za kukabiliana na maadui wanaotaka kupora utajiri wao kwa kuyatenganisha mataifa ya Kiislamu.
Pande hizo mbili pia zilijadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya ulimwengu wa Kiislamu, masuala ya umoja na mshikamano katika safu za wafuasi wa dini hiyo na njama za ubeberu wa kimataifa za kuzusha fitina na hitilafu kati ya Waislamu.
Allamah Fadhlullah amesisitiza juu ya kudumishwa shughuli za Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu Duniani kwa kuzingatia hati ya jumuiya hiyo inayokataza vitendo vya kukufurishana baina ya Waislamu na akasema, haijuzu kuruhusu baadhi ya hitilafu za kifikra katika mitazamo ya elimu ya teolojia na fiqhi ambayo haipingani na misingi ya itikadi za Kiislamu, kuzusha hitilafu na mfarakano kati ya wafuasi wa dini hiyo. 317176