IQNA

Meya wa mji mkuu wa Bulgaria akiri Waislamu wanadhulumiwa

11:54 - November 13, 2008
Habari ID: 1707753
Meya wa Sofia mji mkuu wa Bulgaria Boiko Borisov amekiri kuwa Waislamu wa nchi hiyo walidhulumiwa katika muongo wa 80.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA katika eneo la Balkan barani Ulaya, Borisov ambaye pia ni mkuu wa zamani wa Polisi ya Bulgaria ametoa matamshi hayo katika mdahalo wa televisheni. Akijibu suali la mtangazaji, Borisov amesema kuwa mwanzoni mwa muongo wa 80, serikali ya Bulgaria ilichukua uamuzi wa kutumia mabavu kubadilisha majina yote ya Kiislamu ya Waislamu. Amesema, kikosi cha polisi alichosimamia kilikuwa mojawapo wa taasisi zilizopewa jukumu hilo.
Boiko Borisov ambaye sasa ni kati ya wanasiasa mashuhuri na muhimu wa Bulgaria ameendelea kusema kuwa, alishiriki katika oparesheni ya kuogofya dhidi ya Waislamu na kusema kuwa: 'nadhani nilitekeleza jukumu langu la kiidara ipasavyo na kwa njia bora'.
Matamshi hayo ya Meya wa Sofia yamezua malalamiko makubwa miongoni mwa wananchi mbali mbali na hasa Waislamu wa Bulgaria. Malalamiko hayo yamekuwa makubwa kiasi kwamba mtayarishaji wa kipindi hicho amemtaka meya huyo wa Sofia kurejea tena katika kipindi hicho kwa madhumuni ya kuwaomba radhi rasmi Waislamu kutokana na vitendo na matamshi yake hayo.
Inasemekana kuwa Boiko Borisov amebuni chama kipya cha kisiasa na kwamba anakusudia kugombea kiti cha urais nchini humo.
Mwanzoni mwa muongo wa 80, serikali ya Bulgaria ilichukua uamuzi wa kutumia mabavu kuwalazimisha Waislamu wa Bulgaria kubadilisha majina yao ya Kiislamu. Uamuzi huo ulipelekea kuzuka machafuko katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo ambapo Waislamu wengi waliuawa. Waislamu wa Bulgaria wanalitaja tukio hilo kuwa mkasa wa kihistoria nchini humo. 318543

captcha