Taarifa iliyotolewa na kundi la wanaharakati wa kisiasa na wanasheria wa Misri imeeleza wasiwasi wa wanaharakati hao kuhusu kitendo cha kupeana mikono Sheikh wa al Azhar Muhammad Sayyid Tantawi na Shimon Peres wakati wa mkutano wa Mazungumzo Kati ya Dini Mbalimbali mjini New York Marekani na imetaka kufutwa kazi sheikh wa al Azhar.
Katika upande mwingine hadi sasa Shikh Muhammad Tantawi amekataa kulegeza kamba kuhusu maudhui ya kupeana mkono na Rais wa utawala katili wa Israel unaoendelea kuwaangamiza wananchi wa Palestina wala kuwaomba radhi Waislamu kwa kitendo hicho na amewataja wapinzani wa suala la kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala unaoikalia Quds kwa mabavu kuwa ni waoga na majahili!
Muhammad Tantawi ana uhusiano mkubwa sana na utawala wa Misri. Haki ya kumteua na kumuuzulu Sheikh Mkuu wa Chuo cha al Azhar ambacho ndiyo taasisi kubwa zaidi ya kidini katika ulimwengu wa Kiislamu iko mikononi mwa Rais wa Misri.
Ni vema kukumbusha hapa kuwa picha ya kupeana mikono baina ya Sheikh wa al Azhar na Shimon Peres ilionyeshwa kwa mara ya kwanza tarehe 27 Novemba katika vyombo vya habari vya Misri na kuzusha malalamiko makubwa ya wawakilishi wa bunge na wananchi kwa ujumla.
Mfalme wa Saudi Arabia Abdullah bin Abdulaziz ndiye aliyemwalika Shimon Peres katika mkutano wa Mazungumzo ya Dini Mbalimbali uliofanyika mjini New York Marekani. 328292