IQNA

Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran:

Misaada ya kifedha iliyotolewa na baadhi ya viongozi wa Kiarabu kugharimia mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza ni fedheha ya milele

12:05 - January 10, 2009
Habari ID: 1728822
Hatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa ya mjini Tehran amesema viongozi wa nchi za Kiarabu wameshiriki katika faili jeusi la jinai zinazofanyika katika Ukanda wa Gaza na kwamba baadhi ya nchi hizo zimegharimia mashambulizi ya Israel huko Gaza jambo ambalo litakuwa fedheha ya milele kwao.
Ayatullah Ahmad Khatami amesema kuwa matukio ya Ukanda wa Gaza yamewaumiza walimwengu na kuwatia majonzi makubwa. Amesema, kinachoshuhudiwa hivi sasa katika Ukanda wa Gaza si vita bali ni ukatili na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia hususan watoto na wanawake na kwamba hii leo kama kuna mtu anayetaka kumuona Yazid bin Muawiya aliyemuua Imam Hussein bin Ali (as) katika medani ya Karbala anapaswa kuwatazama Wazayuni wa Israel.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran amesema kuwa Marekani ndiye mshirika mkuu katika jinai zinazofanyika Ukanda wa Gaza na akaongeza kuwa, jinai za Gaza zinafanyika kwa msaada na himaya ya Rais George Bush. Amesema: Kiongozi huyo anahitimisha utawala wake kwa kutenda jinai. na mauaji ya Wapalestina zaidi ya mia nane yatasajiliwa katika faili jeusi la kiongozi huyo.
Amezikosoa pia nchi za Ulaya kwa kunyamazia kimya jinai za Israel huko Gaza na kwamba baadhi ya nchi za bara hilo zimeunga mkono mauaji ya utawala huo ghasibu.
Ayatullah Khatami amesema kwamba baadhi ya nchi za kiarabu zimegharimia mashambulizi ya Israel dhidi ya wananchi wa Gaza na kuongeza kuwa: Inasikitisha kuona kwamba nchi jirani na Gaza imekuwa balaa kwa wakazi wa eneo hilo na inafanya ujasusi kwa maslahi ya Israel badala ya kuwasaidia wa Palestina. Ameongeza kuwa baadhi ya nchi hizo za Kiarabu zimepiga marufu maandamano ya kupinga jinai za Israel dhidi ya wananchi wa Gaza na badala ya kuwasaidia watu wanaodhulumiwa zinashirikiana na madhalimu huku mufti wao msaliti akiyataja maandamano dhidi ya Israel kuwa ni ufisadi. Amewataka watawala wa Misri kutofungamanisha hatima yao na ya Wazayuni na kuwataka wafungue haraka kivuko cha Rafah ili kuwasaidia ndugu zao wa Palestina wanaoteseka chini ya mzingiro na mauaji ya umati yanayotekelezwa na Wazayuni.
Amesema kuwa jinai zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza ni doa jeusi ambalo litaendelea kubaki katika historia dhidi ya watawala wa Israel. Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema kuwa mauaji yanayotekelezwa na utawala huo huko katika Ukanda wa Gaza ni ya kutisha na kusikitisha, na hasa ikitiliwa maanani kwamba, wanawake na watoto wadogo ndio wanalengwa kwa makusudi na askari katili wa Israel.
Ayatullah Khatami amesema kuwa, muhusika halisi wa mauaji hayo ya kutisha ni Marekani, na kuongeza kuwa, kama kungekuwepo mfumo adilifu duniani, watawala wa Israel wangepewa adhabu kali mno. Ayatullah Khatami amelaani kimya cha jumuiya muhimu za kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa ambao una jukumu la kulinda amani duniani, na amezilaumu kwa kuzembea katika kukomesha jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya wakazi wasio na hatia wa Gaza. Amesema kuwa Baraza la Usalama ambalo liliundwa kulinda amani na usalama wa Kimataifa limekuwa baraza la nchi kadhaa duniani na sasa wanadamu wanapaswa kuunda umoja mpya wa kimataifa. 345184
captcha