Wamesema katika taarifa hiyo kwamba, utawala wa Israel umebadili maeneo mawili ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza kuwa jela mbili kubwa dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Wahadhiri hao ambao ni kutoka katika vyuo vikuu vya Manchester, London, Oxford, Leads, Glasgow, York na Cardiff wamesema katika taarifa hiyo kwamba, mauaji ya umati ambayo yamekuwa yakifanywa na utawala wa Israel huko katika Ukanda wa Gaza ni katika mzunguko uleule wa jinai ambazo umekuwa ukizitekeleza dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika kipindi cha miaka 60 ya umri wake.
Taarifa hiyo inaeendelea kusema kuwa, kupitia mauaji hayo yasiyo na huruma na kuwatia hofu na woga Wapalestina, utawala haramu wa Israel unajaribu kuzuia juhudi za Wapalestina za kurejesha haki pamoja na ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, jambo ambalo linawaandalia utangulizi wa kubuni taifa lao huru. Wahadhiri hao wamesisitiza kwamba, jinai za hivi sasa za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi ukiwemo utumiaji wa mabomu yaliyopigwa marufuku kimataifa, ni katika mbinu za kijeshi za utawala huo zisizoambatana na maadili ya kijeshi yanayotambulika kimataifa. Wahadhiri hao wamebainisha masikitiko yao makubwa dhidi ya watu wanaodai kwamba Hamas ndiyo inayosababisha maafa dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na kusisitiza kwamba, utawala haramu wa Israel ndio muhusika mkuu wa jinai hizo zinazotekelezwa dhidi ya wanawake na watoto wadogo wasio na hatia. Wahadhiri hao wa Uingereza wanasema kuwa, hatua za muda tu za Israel kama vile za kusimamisha mapigano na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingizwa katika Ukanda wa Gaza hazitoshi na kwamba jamii ya kimataifa inapasa kuwasaidia Wapalestina katika kurejesha haki zao kukiwemo kutetea ardhi zao na kusimama imara katika kukabiliana na mashambulio ya kichokozi ya utawala huo.
Taarifa hiyo imesema kuwa, ni haki ya kiutu kwa Wapalestina kupambana dhidi ya uchokozi wa Israel na kuwatetea wananchi wao katika Ukanda wa Gaza na kwamba watawala wa Israel wanapasa kutambua vyema kwamba kudhaminiwa usalama wao kunafungamana na kutoka kwa askari wa utawala huo katika ardhi za Wapalestina na kuishi kwao kwa amani na majirani zao. Imesisitiza kwamba utawala wa Israel unapasa kufahamu kuwa usalama wake hauwezi kudhaminiwa kupitia njia za kijeshi.
Taarifa hiyo pia imeitaka serikali ya Uingereza kususia bidhaa za utawala huo na pia kuzuia uwekezaji wa Wazayuni nchini humo. 350367