IQNA

Waranti ya ICC dhidi ya Sudan ni ya kupotosha fikra za waliowengi kuhusiana na udharura wa kuadhibiwa Wazayuni

13:26 - March 08, 2009
Habari ID: 1753155
Waranti iliyotolewa hivi karibuni na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC dhidi ya Rais Omar al-Bashir wa Sudan imelenga kupotosha fikra za waliowengi duniani kuhusiana na udharura wa kufikishwa viongozi wa utawala ghasibu wa Israel katika mahakama hiyo kwa kuhusika kwao na jinai pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu katika Ukanda wa Gaza.
Hayo yamesemwa na Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Akizungumza na Rais Omar al-Bashir katika safari yake aliyofanya nchini humo hivi karibuni, Dakta Ali Larijani amesema kuwa Sudan ni moja ya nchi muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu na kwamba Waislamu wanasifu msimamo wake wa kupambana na siasa za nchi za kibeberu za Magharibi.
Amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kwamba badala ya hatua muhimu kuchukuliwa kwa lengo la kuwaadhibu watawala wa Kizayuni waliohusika na jinai dhidi ya binadamu katika mashambulio yao ya kinyama ya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza, madola hayo yenye kiburi ya Magharibi yamekuwa yakitoa mashinikizo ya kidhulma dhidi ya waungaji mkono wa mapambano ya Kiislamu katika nchi za Palestina na Lebanon.
Amesema katika kipindi cha kufanyika kikao cha Tehran kwa ajili ya kuunga mkono taifa madhlumu la Palestina, washiriki wa kikao hicho waligundua kwamba kulikuwepo na njama zilizokuwa zikifanywa kwa makusudi na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani dhidi ya serikali ya Sudan na kwa hivyo washiriki hao walichukua uamuzi wa haraka wa kupitisha azimio la kuiunga mkono nchi hiyo dhidi ya njama hizo.
Spika wa Bunge la Iran amesema, waliamua kuelekea nchini Sudan ili kutangaza wazi uungaji mkono na mshikamano wao na nchi hiyo katika kukabiliana na njama za nchi za Magharibi. 373943
captcha