Ayatullah Khamenei ambaye alikuwa akihutubia viongozi wa nchi na shakhsia wa kielimu na kisiasa amasema: "Kufuta athari za Kiislamu, matukio ya Haram ya Nabii Ibrahim na kufukuzwa Waislamu katika nyumba zao ni njama hatari mno ambayo inafanyika mbele ya watu wote huku dunia ya Kiislamu ikijishughulisha na masuala madogomadogo." Amesema kuwa ulimwengu wa Kiislamu una uwezo mkubwa wa kukabiliana na tamaa na jinai za Wazayuni na akaongeza kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ambayo kimsingi iliundwa kwa shabaha ya kutetea Palestina, inapaswa kutekeleza wajibu wake wa kuilinda Palestina na kuuhamasisha ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na maudhi ya Wazayuni.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jitihada kubwa zinazofanywa na nchi za Magharibi kwa ajili ya kuondoa dini katika maisha ya mwanadamu na kueneza masuala yaliyodhidi ya maadili na akasema kuwa: "Matokeo ya jitihada hizo ni kusambaratika familia na kuporomoka mahusiano ya watu katika jamii za Magharibi; hata hivyo baada ya kuthibitika ubatili wa fikra hiyo na kugonga ukuta watu wameanza kurejea tena kwenye mafundisho ya dini na sasa Uislamu unapewa mazingatio makubwa kutokana na kuanza harakati hii kubwa."
Ayatullah Khamenei amesema kuwa Uislamu ni kito kinachong'ara na asili katika mfumo wa masuala ya kimaanawi duniani. Ameongeza kuwa hiyo ndiyo sababu kuu ya upinzani uliopo dhidi ya Uislamu. 558715