IQNA

Katibu Mkuu wa ISESCO asisitiza udharura wa kupambana na tatizo la kutojua kusoma na kuandika

17:19 - September 06, 2010
Habari ID: 1988965
Abdul Aziz Othman al-Tuwaijri, Katibu Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ISESCO ametoa taarifa kwa mnasaba wa siku ya kimataifa ya kupambana na kutojua kusoma na kuandika duniani na kusisitiza umuhimu wa mapambano hayo katika nchi za Kiislamu.
Kwa mujibu wa tovuti ya ISESCO, al-Tuwaijri amesisitiza katika taarifa hiyo juu ya ulazima wa kuimarishwa juhudi za kupambana na kutojua kusoma na kuandika kwa ajili ya kunyanyua hali ya jamii za Kiislamu na kupunguza umasikini na ujahili katika jamii hizo. Katibu Mkuu wa ISESCO amesema kwamba kutojua kusoma na kuandika ni tatizo kubwa ambalo linautatiza ulimwengu wa Kiislamu na kikwazo kikubwa katika njia ya kuimarika jamii za Kiislamu katika nyanja zote.
Amesema utafutaji elimu ni jukumu la kidini, kimaadili na kijamii ambalo linapasa kuzijumuisha sekta zote za jamii, serikali na mashirika yote ya kitaifa na kiserikali. Amesema elimu ni jambo linalopaswa kuchukuliwa kuwa ni haki ya kila mtu katika jamii za Kiislamu na kuongeza kuwa hilo ni moja ya malengo muhimu ya ISESCO katika mipango yake ya miaka 2010-2012. 649185
captcha