IQNA

Mkusanyiko mkubwa zaidi wa Waislamu nchini Bangladesh

10:42 - January 24, 2011
Habari ID: 2069083
Mkusanyiko mkubwa zaidi wa Waislamu baada ya ule wa hija ulioanza siku ya Ijumaa tarehe 21 huko katika ukingo wa Mto Turag pembeni ya Dhaka mji mkuu wa Bangladesh ulikamilisha shughuli zake jana.
Waislamu wapatao milioni mbili walikusanyika na kuswali pamoja. Mkusanyiko huo au kwa jina jingine Ijtimai uliendelea kwa muda wa siku tatu. Mkusanyiko huo mkubwa wa Waislamu kutoka nchi 100 za dunia na ambao ulimalizika Jumapili ulifanyika katika uwanja wenye ukubwa wa hekari 66.7.
Mkusanyiko huo ambao hufanyika nchini humo kila mwaka ulianzishwa mwaka 1960 kwa ajili ya kuwawezesha Waislamu kuswali, kusoma Qur'ani na kusikiliza kwa pamoja hotuba za wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu.
Mwaka uliopita Waislamu zaidi ya milioni nne walikusanyika nchini humo kwa ibada hiyo. Hutuba hutolewa kwa lugha tofauti zikiwemo za Kiarabu, Kibangali, Kiingereza, Kiurdu na Kihindi. Mkusanyiko huo ambao huandaliwa na Taasisi ya Uhubiri wa Kiislamu hufanyika kwa lengo la kuwanasihi Waislamu wafuate misingi na mafundisho ya dini yao.
Waislamu wanaunda karibu asilimia 90 ya watu milioni 144 wa Bangladesh. 734685
captcha