IQNA

Ukosefu wa Umoja umewapa wakoloni fursa ya kuwadhibiti Waislamu

14:23 - February 20, 2011
Habari ID: 2083583
Spika wa Bunge la Iran Ali Larijani amesema kuwa ukosefu wa umoja na mwamko na vilevile kuhodhi nchi za Magharibi teknolojia ni mambo ambayo yamedhoosha Waislamu na kuwafanya wadhibitiwe na Wamagharibi.
Akihutubia kongamano la 24 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu lililoanza Februari 19 mjini Tehran Larijani amesema, hii leo ulimwengu wa Kiislamu unahitajia umoja na mshikamano kuliko wakati wowote mwingine. Dakta Larijani ameashiria umuhimu wa umoja baina ya Waislamu na kuutaja kuwa ndio silaha bora ya kukabiliana na maadui wa Uislamu. Larijani amesema mwamko unaoshuhudiwa katika ulimwengu wa Kiislamu unatokana na kufuatia mafundisho ya Mtume SAW.
Kwa upande wake, Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri, Katibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu ameashiria wimbi kubwa la mwamko wa Kiislamu katika pembe mbalimbali duniani na vuguvugu la mapinduzi ya wananchi kaskazini mwa Afrika ambalo hadi sasa limeshawaangusha mataghuti na madikteta wawili wa Tunisia na Misri na kubainisha kwamba, muda si mrefu kutashuhudiwa bendera ya kalima ya tauhidi ikipepea kutoka Asia hadi mashariki na magharibi mwa Afrika.
Maudhui kuu ya mkutano wa sasa wa Umoja wa Kiislamu wa Tehran ni 'Mikakati ya Kifikra na Kivitendo ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu. Shakhsia 250 kutoka nchi 57 duniani wanashiriki katika kongamano hilo ambalo hufanyika kila mwaka kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu.
750350
captcha