IQNA

Mkuu wa wanazuoni wa Kisuni wa Kusini mwa Iraq alalamikia filamu ya Muawiyya, Hassan na Hussein

21:44 - August 12, 2011
Habari ID: 2168899
Khalid al-Mulla, Mkuu Jumuiya ya Wanazuoni wa Kisuni wa Kusini mwa Iraq amelalamikia vikali urushwaji hewani filamu iliyo dhidi ya Ushia inayoitwa 'Muawiyya, Hassan na Hussein' kupitia televisheni za satalaiti na kutaka filamu hiyo isimamishwe mara moja katika Televisheni ya Baghdad.
Akitoa taarifa kuhusiana na suala hilo, Khalid al-Mulla ameonya dhidi ya mifarakano na fitina za kimadhehebu zinazoweza kuzushwa na filamu hiyo katika jamii ya Kiislamu.
Baadhi ya wanazuoni wa Kisuni wameharamisha filamu hiyo kwa sababu inachochea chuki, uadui na fitina kati ya Waislamu. Khali al-Mulla amezitaka televisheni zote za satalaiti kujiepusha kuonyesha filamu na vipindi vinavyochochea chuki na mifarakano ya kimadhehebu pamoja na kubeza matukufu ya Kiislamu na vilevile kuwataka wanazuoni wa Kiislamu kutekeleza majukumu yao vyema kwa kuepusha fitina miongoni mwa Waislamu.
Filamu ya 'Muawiyya, Hassan na Hussein' imekuwa ikirushwa hewani na kanali kadhaa za televisheni za satalaiti tokea mwanzoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Licha ya malalamiko hayo ya Waislamu lakini Yusuf al-Qardhawi, mkuu wa Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu amejuzisha kuonyeshwa kwa filamu hiyo inayokosea heshima matukufu ya Kiislamu.
Katika upande wa pili, Mansur Shariff, Mkuu wa Jumuiya ya Masharifu wa Misri amepinga vikali filamu hiyo na kuwataka wananchi wa nchi hiyo wafanye maandamano makubwa dhidi yake katika Medani ya Tahrir ili kuwalazimisha wahusika waisimamishe mara moja. Amesema, kuonyeshwa filamu hiyo ni dharau ya moja kwa moja kwa watukufu wawili hao waliobashiriwa Pepo na waliopewa malezi ya moja kwa moja na Mtume Mtukufu (saw). 840942
captcha