Akizungumza hapo jana Jumamosi, Hania amesema kwamba mapinduzi ya wananchi Waislamu wa Misri hayakuwa na faida kwa nchi hiyo pekee bali yameziathiri pia nchi nyingine za eneo ikiwemo Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Ameashiria matukio ya Misri na kusisitiza kwamba anaamini kuwa nchi hiyo ya Kiislamu inahuisha nafasi yake muhimu iliyokuwa nayo katika Mashariki ya Kati. Amegusia pia uhusiano uliopo kati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas na kundi la Ikhwanul Muslimin la Misri na kusema kuwa Hamas inatokana na kundi hilo muhimu la Kiislamu kwa sababu wanachama wake wengi walipewa mafunzo na malezi na kundi hilo.
Amesema kuwa Wapalestina wanaupa umuhimu mkubwa usalama wa Misri na kwamba walichukua hatua maalumu za kuimarisha usalama wa mpaka wa pamoja wa nchi hizo katika kipindi cha kufanyika mapinduzi ya Wamisri dhidi ya utawala wa dikteta Hosni Mubarak.
Hania pia amezungumzia suala la nishati inayotumika katika Ukanda wa Gaza na kusema kuwa Misri ndiyo inayodhamini nishati hiyo yote na kwamba ni Mamlaka ya Ndani ya Palestina ndiyo inayojaribu kuvuruga ufikishaji wa nishati hiyo katika ukanda huo kwa dhana kwamba huenda suala hilo likauunganisha ukanda huo na Misri jambo ambalo amesisitiza halina msingi. 880545