Katibu Mkuu wa shirika la Kiislamu la Elimu, Sayansi na Utamaduni (ISESCO) amesema katika ujumbe wake wa salamu za idi kwamba somo kubwa zaidi la Idul Adh'ha ni ulazima wa kufuata amri za Mwenyezi Mungu katika hali zote.
Abdulaziz Othman Al-Tuwaijri ameuambia umma wa Kiislamu kwamba Waislamu kote duniani wanapaswa kupata ilhamu ya somo kuu la Idul Adh'ha na kumuiga Nabii Ibrahim (as) kwa kufuata amri za Allah (sw) katika kila hali.
Amesema kuwa idul Adh'ha inapaswa kuwa mwanzo wa Waislamu kutoa kipaumbele kwa suala la umoja na mshikamano na kujiepusha na hitilafu na mifarakano inayodhoofisha umma wa Kiislamu.
Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake wa idi, Katibu Mkuu wa ISESCO amesema kuwa ushirikiano wa kudumu kati ya nchi za Kiislamu katika nyanja mbalimbali ndio njia pekee ya kupata nguvu katika medani za kimataifa. Amesema Waislamu wanapasa kuelewa kwamba hawawezi kufikia malengo yao kama hawatakuwa na umoja na mshikamano.
Al Tuwaijri amesisitiza juu ya udharura wa Waislamu kuelewa matatizo ya dunia ya sasa na kwamba kuelewa matatizo ya dunia kutawawezesha Waislamu kutambua vizuizi vya maendeleo ya ulimwengu wa Kiisalmu na kutafuta ufumbuzi wake. 893873